WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema haijaridhishwa na kiwango cha ufaulu wa wanafunzi kwa mitihani ya kidato cha pili na cha nne na kuwataka walimu kubuni mikakati ya kuongeza ufaulu.
Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Mmanga Mjengo Mjawiri alisema hayo wakati akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Jumbi wilaya ya Kati Unguja baada ya kufanya ziara kuangalia maendeleo ya sekta hiyo pamoja na matayarisho ya mitihani ya taifa.
Mjawiri alisema kiwango cha ufaulu usioridhisha kimewavunja moyo wazazi wengi ambapo moja ya kazi kubwa ya Wizara ya Elimu ni kulipatia ufumbuzi suala hilo kwa haraka.
“Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesikitishwa na matokeo mabaya ya mitihani ya wanafunzi wa kidato cha pili na cha nne na sasa imeanza kufanya utafiti zaidi kujua chanzo chake na juhudi za kukabiliana nazo,” alisema.
Aliwataka walimu kuhakikisha wanakamilisha mitaala ya masomo yao kwa ajili ya maandalizi mazuri ya mitihani kwa wanafunzi na katika maandalizi wanatakiwa kuhakikisha kwamba masomo yaliyomo katika mitaala yanafundishwa na kukamilika kwa ajili ya matayarisho ya mitihani ya taifa.
Katika kufanikisha suala hilo, walimu wakuu wametakiwa kufanya ukaguzi mara kwa mara kwa walimu wote ili kuhakikisha kila mwalimu anatekeleza majukumu yake kikamilifu kwa wakati.
Mjawiri aliwataka walimu wa Jumbi kufanya kazi kwa kuzingatia maadili na nidhamu na kusema serikali ipo katika hatua za kuyapatia ufumbuzi malalamiko ya walimu yakiwamo malimbikizo ya madai yao ambayo yatatekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2016/2017.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Jumbi, Maimuna Ilyasa alisema wamefanikiwa kudhibiti utoro kwa wanafunzi ambao hujishughulisha na ajira.
Wanafunzi wa kidato cha pili na nne wa shule za sekondari za Unguja na Pemba wapo katika maandalizi ya mitihani ya taifa ambayo inatazamiwa kufanyika mwezi ujao.
Takwimu za wizara, zinaonesha kwamba ufaulu wa wanafunzi kwa mitihani ya kidato cha nne hadi cha sita inayotayarishwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) umeshuka kwa asilimia 30.
|
0 Comments