|
VIWANDA 22 vinatarajiwa kujengwa nchini na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, ikiwa ni utekelezaji wa mwito wa Serikali wa kuzitaka hifadhi ya jamii kuwekeza na kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda nchini.
Katika utekelezaji wa agizo hilo, mifuko ambayo imeshaanza utekelezaji ni NSSF, PPF, PSFP, LAPF, GEPF wakati Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) nao tayari umeanza kufanya mapitio ya kina kwa ajili ya kuwekeza katika uzalishaji maeneo mbalimbali, yenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa dawa hospitalini.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (TSSA), Meshack Bandawe alisema jana mjini hapa kuwa hatua hiyo ya mifuko ya hifadhi ya jamii ya kujikita katika uwekezaji wa viwanda, itasaidia asilimia 40 ya ongezeko la ajira nchini itokane na sekta ya viwanda.
Alikuwa akizungumza katika mkutano wa sita wa wadau wa mfuko wa NSSF, unaofanyika mjini hapa.
Katika uwekezaji huo, PPF imeanza mchakato wa ujenzi wa jengo la uzalishaji kwa ajili ya kampuni ya nguo ya TOOKU na kiwanda hicho kinajengwa katika eneo huru la kiuchumi la Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mfuko huo pia utapanua kiwanda cha viatu cha magereza kilichoko Karanga mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na Jeshi la Magereza na pia watafanya kwa ubia na NSSF katika kujenga kiwanda cha sukari huko Mkulazi mkoani Morogoro.
Bandawe alisema mfuko wa PSPF utajenga eneo maalumu la kiuchumi katika eneo la Kurasini, ambako kitakuwa ni kituo cha bidhaa zinazotoka China na itajenga kiwanda cha kutengeneza Agave Syrup kutokana na mabaki ya mkonge mkoani Tanga.
Mfuko wa LAPF utafufua Kiwanda cha Chai cha Mponde kilichoko Lushoto, Tanga na watajenga kiwanda cha kutengeneza bidhaa za hospitali na majitiba. Kwa upande wa Mfuko wa GEPF utafanya mradi wa ujenzi na ufufuaji wa kiwanda cha kuchonga vipuri katika eneo la Kilimanjaro Machine Tools mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.
Mfuko huo pia utajenga machinjio ya kisasa kwa kushirikiana na Kampuni ya Ranchi za Taifa (Narco) na Benki ya Uwekezaji (TIB) huko Tandahimba, Mtwara na kujenga kiwanda cha kusindika juisi na mvinyo utokanao na zabibu huko Chinangali mkoani Dodoma na watafufua na kuendeleza kiwanda cha kubangua korosho cha Tandahimba mkoani Mtwara.
Shirikisho la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (TSSA) wao wamejipanga kufufua na kuendeleza uanzishwaji viwanda vipya vya sekta ya nguo na mavazi, ufufuaji na uendelezaji wa viwanda vipya vya sekta ya ngozi na bidhaa za ngozi na uanzishwaji wa viwanda vipya vya uchongaji wa vipuri.
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara alisema mfuko wake umedhamiria kuwekeza zaidi kwenye viwanda vya kusindika nafaka pamoja na mafuta ya kula.
Aliongeza kuwa uwekezaji katika maeneo hayo, hauhitaji mitaji mikubwa. Alisema kiwanda cha sukari ambacho wanakijenga kwa ubia na PPF, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha tani 200,000 kwa mwaka na kitatoa ajira kwa watu wapatao 100,000.
Profesa Kahyarara alisema NSSF imejipanga kufufua vinu vya usagaji wa nafaka vya NMC vilivyopo Iringa, Dodoma na Arusha, watafufua kiwanda cha matairi cha Arusha (General Tyre) na pia wanakamilisha uzalishaji wa majaribio wa kiwanda cha viuadudu kilichoko Kibaha, mkoani Pwani.
Mfuko wa NHIF kwa kuanzia unatafanya mradi wa uzalishaji dawa na bidhaa hospitalini, uzalishaji wa maji tiba na uzalishaji wa gesi kwa ajili ya tiba. Kutokana na kujikita katika maeneo hayo, mfuko huo umepanga kufufua viwanda vilivyopo katika hospitali mbalimbali kwa ajili ya utengenezaji wa maji tiba.
Pia watajenga kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa za hospitali kwa ubia na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, watajenga kiwanda cha uzalishaji dawa kali kwa ubia na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), watajenga kiwanda cha uzalishaji wa gesi ya oksijeni katika Taasisi ya Mifupa ya Muhimbili (MOI).
Bandawe alisema mfuko huo, pia utafanya uwekezaji kwa kushirikiana na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kufufua uzalishaji wa dawa katika kiwanda cha dawa kinachomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa cha Mgulani; na kujenga kiwanda kipya kikubwa cha kisasa kwa ajili ya kuzalisha dawa pamoja na bidhaa mbalimbali za hospitali katika kambi ya Ruvu.
Alisema mfuko wa ZSSF umejipanga kuingia katika uvuvi wa bahari kuu na usindikaji wa samaki na kuongeza kuwa mfuko huo uko tayari kushiriki katika miradi ya pamoja itakayotekelezwa na TSSA.
“Miradi yote hii tunashirikiana na Benki ya Azania ambayo mifuko yote ni wabia na tunataka kuifanya benki hii iwe ya viwanda. Pia tutashirikiana na JKT katika utekelezaji wa miradi hiyo,” alisema Bandawe.
Wanachama waonesha wasiwasi
Hatua hiyo ya mifuko kwenda kuwekeza kwenye viwanda, imewafanya wanachama wa NSSF kuonesha wasiwasi kama uwekezaji huo utakuwa na tija mbele ya fedha zao. Walitaka kuwepo na maelezo ya kuridhisha, kwa vile mfuko huo unaenda kuwekeza huko wakati kuna manung’uniko ya uwekezaji katika majengo.
Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama Huru vya Wafanyakazi (TUCTA), Gratian Mkoba alipongeza hatua hiyo kwamba inarudisha sasa mashirika ya umma na Serikal kufanya uwekezaji tofauti na miaka ya nyuma serikali ilijiondoa kwenye kufanya biashara.
Samuel Magelo kutoka Tughe alisema ni jambo zuri kuwekeza lakini akahoji inakuwaje mifuko hiyo, inaenda kuwekeza kwenye viwanda huku baadhi yao imeshindwa kulipa mafao ya wanachama wao, kwa madai kuwa haina fedha.
Geofrey Kemeti alisema wadau wanaonesha wasiwasi wa uwekezaji kwenye viwanda na akahoji fedha hizo zitatoka wapi.
“Mifuko yetu itakuwa salama katika uwekezaji huu? Alihoji. SSRA, Profesa Wangwe watetea Katika kujibu hoja hizo, Mwenyekiti wa Bodi ya NSSF, Profesa Samuel Wangwe alisema kwamba bodi ambayo ina dhamana na uwekezaji huo, wamechukua tahadhari kubwa kuhakikisha kwamba uwekezaji utakaofanyika unaongeza mafao ya wanachama. “Kazi yetu ni kulinda fedha zenu, hilo tunalifanya kwa makini. Na bila kuwekeza mafao hayaweza kuongezeka,” alisema Profesa Wangwe.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa mifuko ya hifadhi (SSRA), Irene Isaka alisema kwamba mifuko ina uhuru wa kuwekeza sehemu yoyote ili mradi wafuate mifumo ya uwekezaji. Aliongeza kuwa mifuko inaweza kuwekeza kwa kununua hisa, majengo au kununua hati fungani na kutoa mikopo.
“Tukisema mifuko inaenda kuwekeza kwenye viwanda, sio kwamba fedha zote watazielekeza huko, ni sehemu tu ya fedha itaelekezwa huko,” alisema Irene na kuongeza kuwa uwekezaji kwenye viwanda utaisaidia mifuko kuongeza idadi ya wanachama.
0 Comments