Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari amejibu onyo kutoka kwa mkewe ambaye alikuwa ametahadharisha kwamba hatamuunga mkono uchaguzi mkuu ujao iwapo hatafanya mabadiliko serikali.
Bi Aisha, kwenye mahojiano na BBC, alikuwa amedokeza kwamba mumewe amepoteza udhibiti wa serikali.
Bw Buhari kwa sasa yumo kwenye ziara rasmi nchini Ujerumani na kwa mujibu wa shirika la habari la AP, amemjibu mkewe wakati wa kikao cha wanahabari akiwa pamoja na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Bw Buhari anaanza kwa kucheka kidogo kisha kusema: "Sijui mke wangu ni wa chama gani, lakini najua yeye ni wa kwangu jikoni na sebuleni na chumba hicho kingine."
Kiongozi huyo aliyeingia madarakani mwaka jana amesema pia kwamba na ujuzi na uzoefu zaidi ya mkewe katika siasa.
Amesema alijaribu kwa miaka 12 kuwa rais na akafanikiwa kwa mara ya nne.
"Kwa hivyo, nina ujuzi kushinda yeye na watu wengine wa upinzani, kwa sababu mwishowe nilifanikiwa. Si rahisi kuridhisha vyama vyote vya upinzani nchini Nigeria au kushiriki serikalini."
Bi Merkel alionekana kushangazwa na matamshi ya Bw Buhari.
0 Comments