WAKATI mchakato wa kumtangaza Rais wa Kwanza wa Tanzania, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kuwa mtakatifu kupitia Kanisa Katoliki duniani ukiendelea, maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 17 ya kifo chake jana, yameendelea kumdhihirisha kiongozi huyo kustahili heshima hiyo ya juu ya kidini.
Kwa mara nyingine jana, Watanzania wamekumbushwa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kurejea misingi ya Azimio la Arusha, inayokataza na kupinga vitendo vya rushwa na kuwataka viongozi wa umma kuwatumikia wananchi kwa utu na si maslahi binafsi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, kwenye kongamano la maadhimisho ya kumbukizi hiyo iliyofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, watoa mada tofauti walitoa mada zinazosisitiza misingi ya Azimio la Arusha na kusema ni lazima lirejewe, ikiwa Tanzania inataka kuendelea.
Akitoa mada kuhusu Maadili ya Viongozi, Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Philip Mangula alisema misingi ndani ya Azimio hilo ni dira ya uelekeo wa nchi na kuwataka viongozi wote kufahamu kuwa wana wajibu wa kuwatumikia wananchi kwa kuzingatia misingi hiyo na si vinginevyo.
“Hali ni tofauti na wakati wa utawala wa Baba wa Taifa. Siku hizi viongozi wa vyama tumeharibika, tunatumia vibaya madaraka na wapiga kura nao wamejigeuza bidhaa, wamejirahisisha na kushusha thamani yao kwa kukubali kununuliwa kama sambusa na kipande cha kuku, hayo ni makosa makubwa, jamii ilifika pabaya,” alisema Mangula.
Alisisitiza kuwa ni lazima viongozi na wananchi wakafahamu kuwa misingi ya Azimio la Arusha ni utu na si kuuza utu wao kwa rushwa ili kumpata kiongozi kwa sababu kufanya hivyo ni kukiuka msingi hiyo na mwisho wa siku huyo aliyechaguliwa kwa rushwa hana sifa za kuwa kiongozi.
Akirejea kauli ya Mwalimu Nyerere, Mangula alisema enzi za Mwalimu, na hata kwenye vitabu mbalimbali alivyoandika kuhusu utawala na siasa, misingi ya Azimio la Arusha ipo na ndio msingi na dira inayopaswa kufuatwa na viongozi wote wenye nia njema ya kuifanya Tanzania isonge mbele kimaendeleo na kuzingatia utu na haki.
Akitoa mfano wa maadili katika kongamano hilo, Mangula alisema hata katika CCM, msingi unaoangaliwa wa kiongozi mwenye sifa za kuongoza ni yule anayefuata misingi ya Azimio hilo na kwamba hata katika uchaguzi uliopita, wananchi mbalimbali waliowania nafasi za uongozi na wakagunduliwa walitoa rushwa, walikatwa majina yao kwa kuwa walikosa sifa.
“Wananiita mbeba mafaili ni kweli, ndani ya chama niko kwenye Kamati ya Maadili na mafaili ya watangaza nia 41 ya urais kwenye uchaguzi uliopita nilikuwa nayo, napekua naangalia na nilipoona baadhi yao wanazidi kwa tuhuma za rushwa niliwaita sita,” alisema Mangula.
Alisisitiza kuwa wote waliohusika kwenye mchakato wa uchaguzi kwa misingi ya rushwa hawakupewa nafasi kwa sababu chama kilishatoa angalizo mapema kuwa ni lazima wagombea wawe wasafi na hiyo pia imeendelea hadi baada ya serikali kuingia madarakani, ambapo chama kilimwagiza rais, kuchukua hatua kwa kutenganisha Sheria ya Biashara na Maadili ya Utumishi wa Umma.
“Ilifika wakati wafanyabiashara wakataka wateke nchi, hao hao ni wanasiasa haohao ni wafanyabiashara, tumesema hapana, lazima vitenganishwe ili kulinda misingi ya Azimio la Arusha inayosisitiza uadilifu iliyoasisiwa na Mwalimu. “Yeyote anayefikiri atatumia fedha akidhani atafanikiwa ndani ya serikali hii, ni vyema akatambua imekula kwake, hakuna nafasi ya fedha katika uongozi huu, msingi mkubwa tumesisitiza ni maadili,” alisema Mangula.
Kwa upande wake, mgeni rasmi Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Mafunzo ya Ufundi, Stella Manyanya alisema ni vyema watanzania na viongozi wote wakarejea misingi ya Azimio la Arusha kwa sababu limeeleza bayana mambo ya msingi ya kufanya, ili nchi ipige hatua kimaendeleo.
“Ni wazi ndani ya Azimio la Arusha ambalo Mwalimu Nyerere katika hotuba zake anasisitiza haoni dosari, ni kweli linapaswa kufuatwa ili kuifanya nchi ikue, na kuachana na masuala ya rushwa na kuzungatia miiko ya maadili,” alisema Manyanya.
Naye mtoa mada kuhusu Miiko ya Uongozi, Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu, Joseph Butiku alisema sifa kubwa ya Mwalimu Nyerere alikuwa muumini mzuri aliyeamini binadamu na kuona wote ni watu na wanastahili kufanyiwa utu, ingawa kila mtu ana tofauti yake.
Butiku alisema miiko ya uongozi iko wazi ndani ya Azimio la Arusha na kwamba yeyote anayetaka kuwa kiongozi hata ngazi ya urais ni lazima awe kiongozi wa watu na si kiongozi anayetaka kufukuzana na fedha kwa maslahi binafsi.
Alisema miiko hiyo ni muongozo mzuri ingawa wapo viongozi wanaojitahidi kukataa ahadi hiyo ya miiko na wamekuwa wakitoka nje ya mstari kwa kuwa wanafahamu hawawezi kuitekeleza kwa sababu wana maslahi yao binafsi kuliko ya umma.
Naye mtoa mada kuhusu Azimio la Arusha, Dk Harun Kondo alisema ingawa wapo watu wanataka Azimio hilo life, ni vigumu kuliua kwa sababu si jambo jepesi lina misingi ya kisayansi, inayoonesha wapi nchi inakwenda na hilo ndio tegemeo pekee la ukombozi wa nchi.
“Wapo watu na hata viongozi wanataka Azimio life, watakufa wao wataliacha Azimio likiendelea, kwa sababu ndio msingi na dira inayoonesha wapi tupo, tunakokwenda, ni ukombozi wetu na ni lazima tulirejee sasa,” alisema Dk Kondo.
Rais Shein ‘alia’ na misaada ya nje
Katika hatua nyingine, Serikali imesema haitapokea misaada yenye masharti kutoka kwa wahisani wa maendeleo inayolenga kuharibu mipango ya maendeleo ya nchi na badala yake itapokea misaada tu yenye kujenga utu na heshima ya nchi ndani na nje ya nchi.
Hayo yalisemwa jana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Barazala la Mapinduzi, Dk Ali Mohamedi Shein alipokuwa akiwahutubia mamia ya wakazi wa Bariadi kwenye kilele cha mbio za Mwenge wa Uhuru, ambapo kitaifa zilizofanyika mjini hapa na kuambatana na kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu.
“Wapo wahisani wa maendeleo ambao hutoa misaada ya masharti kwa ajili ya kuharibu mipango yetu ya maendeleo, hatuko tayari kuipokea misaada ya aina hiyo, wale wanaotutishia tuko tayari kuachana nao,” alisema.
Alisema serikali itakuwa tayari kustahimili na kuacha kuipokea misaada hiyo kuliko kudhalilishwa kwa kupatiwa misaada ya masharti. Dk Shein alisema wapo Watanzania mwenye uchu wa kufanya hujuma na ubadhirifu serikalini na kwenye mali za umma na kuonya kuwa serikali haitawavumilia watumishi wa aina hiyo.
Aliwaonya wale wote wanaoeneza vitendo vya ubadhirifu kwenye mapato ya serikali kwa sasa waache tabia hiyo na kusisitiza kuwa chini ya uongozi wa awamu ya tano unaongozwa na Rais John Magufuli hawatakuwa na nafasi hiyo.
“Taasisi zilizokabidhiwa dhamana ya ukusanyaji wa mapato kwa Tanzania Bara na Visiwani, lazima ziwajibike kikamilifu katika kukusanya mapato na zifanye kazi kwa karibu naTaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kudhibiti mianya ya rushwa,” alifafanua.
Alimpongeza Rais Magufuli kwa jinsi alivyojenga maadili ya utumishi wa umma serikalini na kuwafanya watumishi wa umma kutekeleza majukumu yao kama inavyostahili.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama alisema Mwenge wa Uhuru, mwaka huu ulizindua na kuweka mawe ya msingi katika jumla ya miradi 1,387 yenye thamani ya Sh bilioni 498.8 ambayo imeanza kutoa huduma kwa wananchi.
Mchakato Mwalimu Nyerere kuwa Mtakatifu
Wakati mchakato wa kumfanya Mwalimu Nyerere kuwa Mtakatifu, hivi karibuni Rais Yoweri Museveni wa Uganda, alisema kiongozi bora ni yule anayefuata maagizo ya Mungu na kuwatumikia binadamu wote kwa usawa na haki.
Aliyasema hayo wakati wa Ibada ya kuombea mchakato wa kumfanya Nyerere kuwa Mwenyeheri na hatimaye kutangazwa Mtakatifu.
Alisema hata kwenye maandiko matakatifu ya Biblia, kuna mistari inayomtaka binadamu ampende binadamu mwenzake kama anavyojipenda yeye.
“Kwenye Biblia kuna sehemu inauliza kuwa utampendaje Mungu ambaye hujawahi kumuona, na ushindwe kumpenda binadamu mwenzako?” alisema Museveni. Alisema kwa sababu aliwahi kufanya kazi na Mwalimu, anaweza kutoa ushahidi kwamba Mwalimu alifanya yote mawili - kumtii Mungu na kuwatumikia binadamu.
Alisema mojawapo ya sababu iliyomfanya aliyekuwa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Dunia, marehemu Papa Paulo II kutangazwa mtakatifu ni kuisaidia Ulaya Mashariki, ambayo wananchi wake walikuwa hawamwamini Mungu.
“Papa Paulo II alisaidia kuikomboa Ulaya Mashariki kutoka kwenye ukomunisti, wananchi walikuwa hawaamini kuna Mungu, lakini kwa juhudi zake aliwafanya wamwamini na kumpenda Mungu,” alisema.
Rais Museveni alisema anatarajia kupeleka ushahidi kwa Kiongozi wa sasa wa Kanisa hilo duniani, Papa Benedict kwamba Mwalimu ana sifa za kutangazwa kuwa Mtakatifu kwa sababu alimtii Mungu na kuwatumikia binadamu.
“Mimi nitapeleka ushahidi kwa Papa, kwamba mbali na Mwalimu kumtii Mungu na kuwapenda binadamu wote, pia aliwakomboa Waafrika kutoka Ruvuma mpaka Capetown nchini Afrika Kusini, huu ni ukweli, si hadithi,” alisisitiza Rais Museveni.
Habari hii imeandikwa na Ikunda Erick, Dar na Nashon Kennedy, Simiyu
|
0 Comments