SIKU moja baada ya viongozi mbalimbali akiwemo Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi kuonya nchi kupoteza mwelekeo miaka 17 baada ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, imeelezwa kuwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli ameanza kurejesha misingi hiyo.
Mwinyi na viongozi wengine akiwemo pia Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba wakizungumza kwenye midahalo ya Kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere juzi, walieleza shaka juu ya nchi kuanza kumeguka katika misingi ya ukabila na udini, hatua waliyosema inatishia umoja na mshikamano wa kitaifa.
Akizungumzia hofu hiyo jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Jamii kwa Madhehebu ya Dini nchini, Askofu William Mwamalanga alisema Rais John Magufuli ameanza kuirejesha nchi katika misingi yake.
“Ni vizuri kueleza hofu iliyopo lakini ni vizuri zaidi kutambua jitihada zinazochukuliwa na Rais wa sasa Magufuli katika kurejesha nchi katika misingi ya Azimio la Arusha ambayo iliweka misingi ya uongozi. “Hili lipo wazi, Mwalimu alikemea rushwa na watu waliogopa rushwa sawa na sasa ambapo hofu ya rushwa ipo tofauti na ilivyokuwa hapo katikati. Rais Magufuli amechukua hatua nyingi kama kuhimiza uwajibikaji na kukemea matumizi mabaya ya madaraka kama ilivyokuwa wakati wa Mwalimu,” alisema Askofu Mwamalanga.
Alisema mbali ya kurejesha misingi ya uongozi, Rais Magufuli pia ameweza katika kipindi cha muda mfupi kujenga heshima ya nchi ya Tanzania nje, kutokana na na jitihada zake za kutetea wanyonge, kuheshimu utu wa mtu, kuhamasisha umoja na mshikamano, kukemea rushwa, kulinda maliasili za nchi, kuhamasisha nchi na Mataifa ya Afrika kujitegemea na kukataa misaada yenye masharti yasiyo na staha kwa Taifa kama alivyofanya Mwalimu Nyerere.
“Ukiangalia kwa makini ni sawa na kusema Rais Magufuli amerithi utashi wa kisiasa wa Mwalimu Nyerere, nionavyo ni vema tukazitambua jitihada anazozifanya katika kuziba nyufa zilizoainishwa na viongozi wetu wakati wa Kongamano la Mwalimu,” alisema.
Aidha kiongozi huyo wa dini alisema Rais Magufuli ameanza kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti ukabila na udini na kuhamasisha umoja wa kitaifa, ikiwa ni pamoja na kujaribu kuondoa pengo kubwa lililojengeka kwa miaka kadhaa baada ya kifo cha Nyerere baina ya tabaka la watu wenye nazo na wasio nacho.
“Ukubwa wa pengo la kipato kati ya wenye nacho na wasio nacho ambao ulikuwa umekua kwa kiwango kikubwa katika miaka ya hivi karibuni sasa umeanza kupungua. Ni imani yangu kwamba miaka michache ya uongozi wa Rais Magufuli, watu wataheshimiana na kuwa wamoja kutokana na kugawana sawa rasilimali za Taifa,” alisema.
|
0 Comments