Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akihutubia wakazi wa Mlandizi mkoani Pwani akiwa njiani kuelekea mkoani Dodoma. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais) |
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameandika historia ya aina yake kwenda Dodoma kufanya ziara, ambapo ametumia njia ya barabara na kufanya mikutano kadhaa katika mikoa yote ya njiani ya Pwani na Morogoro.
Mtindo huo wa viongozi wa juu wa Serikali ya Awamu ya Tano, kusafiri kwa njia ya barabara, uliasisiwa na Rais John Magufuli ambaye mara kadhaa amesafiri kwenda Dodoma kwa njia ya barabara, safari ya umbali wa zaidi ya kilometa 470.
Jana ilikuwa ni zamu ya Makamu wa Rais, ambapo njiani alifanya mikutano na wananchi katika miji ya Chalinze na Mlandizi mkoani Pwani, Msamvu mjini Morogoro na Gairo mkoani Morogoro.
Pamoja na kuzungumzia matatizo ya kimaeneo, safari ya barabara ya Makamu wa Rais jana ilibebwa na ujumbe mkubwa wa hatua zinazochukuliwa na serikali katika kukabili mapigano baina ya wakulima na wafugaji, yaliyoshamiri katika mikoa ya Pwani, Morogoro, Dodoma na Manyara.
Mkutano wa Chalinze
Akiwa Chalinze, Samia alisema ardhi isiwe chanzo cha umwagaji damu kutokana na mapigano ya wakulima na wafugaji. Bali, kila upande unapaswa kusimamia sheria na taratibu ili kuepusha hali hiyo; huku serikali ikiendelea na mipango ya kupima maeneo.
Alisema hivi sasa kumekuwa na migogoro ya wakulima na wafugaji, ambayo imesababisha vurugu, ambazo zinasababisha umwagaji wa damu, jambo ambalo serikali haitaki kuliona na kutaka kila upande kuheshimu sheria.
“Hatutaki kusikia migogoro hii inaendelea na halmashauri, Mkuu wa Wilaya na Mkoa kaeni tengenezeni utaratibu kuondoa kasoro zilizopo ili watu waweze kuishi kwa amani, kwani hakuna haja ya kuendelea kusikia malumbano ambayo hayana faida,” aliagiza Samia.
Alisema tataizo lingine ni baadhi ya wafugaji, kuwatumia watoto kuchunga mifugo na matokeo yake ni kushindwa kuidhibiti mifugo hiyo kuingia shambani na kufanya uharibifu wa mazao na kusababisha migogoro hiyo.
“Mnapaswa kuwapeleka watoto wenu shule, kwani elimu ndiyo urithi wa watoto wenu, kwani kwa sasa kutakuwa na uwekezaji mkubwa katika mkoa wa Pwani, ikiwa ni pamoja na viwanda vya bidhaa zitakazotokana na mifugo na ajira zitapatikana, kama watoto wenu hawajasoma hawatafaidi uwekezaji huo,” alisema Makamu wa Rais.
Akizungumzia kero ya maji, kufuatia ombi la Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete (CCM) ambaye alisema kuna tatizo kubwa la ukosefu wa maji katika mji huo, jambo ambalo limekuwa kero kubwa, Makamu wa Rais alisema suala hilo linashughulikiwa.
“Kwa sasa fedha zimetengwa shilingi bilioni 43 kwa ajili ya kusambaza maji kutoka Mto Wami ambako kutajengwa matangi kwenye baadhi ya maeneo. Eneo la Pera litajengwa tangi la kuhifadhi lita 300,000, Kibiki lita 200,000 na tangi lingine kubwa litakalokuwa na uwezo wa kuhifadhi lita milioni 2 na tunatarajia ifikapo mwishoni mwa mwaka huu matokeo yataonekana,” alisema Samia.
Akiwa mji wa Mlandizi wilayani Kibaha, alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itatekeleza ahadi zote ilizoahidi ili kuwaondolea kero wananchi, ikiwa ni pamoja kwenye sekta zote ili kuhakikisha maendeleo yanawafikia wananchi.
Mkutano wa Morogoro
Akiwa mkoani Morogoro katika eneo la Msamvu ndani ya Manispaa ya Morogoro na pia Gairo, Makamu wa Rais alielezea mikakati mbalimbali ya serikali katika kukabili tatizo la mapigano baina ya wakulima na wafugaji na pia kuhusu kukabili tatizo la maji mkoani Morogoro.
Alisema kuwa serikali isingependa kusikia tena kutokea kwa mauaji ya wakulima na wafugaji nchini na hasa katika mkoa huo.
Aliwataka wafugaji wote nchini wakiwemo wa mkoani Morogoro, kutii agizo la kisheria la utambuzi na upigaji chapa ng’ombe; wale watakaokaidi, mifugo yao haitaruhusiwa kupelekwa minadani kuuzwa na kwamba wafugaji wanatakiwa kutii Sheria hiyo Namba 12 ya Mifugo ya Mwaka 2010.
Alisema haina maana wala tija kwa wafugaji, kufanya mgomo wa kuchinja ng’ombe kwa kutaka kushinikiza Sheria ya Utambuzi na Upigaji Chapa isitekelewe kwa Mkoa wa Morogoro.
Pamoja na hayo, alisema Serikali ya Awamu ya Tano itatekeleza ahadi zote zilizotolewa wakati wa Uchaguzi Mkuu uliopita hatua kwa hatua na kwamba kwa kuanzia imeanza kurudisha nidhamu ya utumishi wa umma. Pia aliwataka vijana wajitume kufanya kazi, kwa vile serikali inaweka mazingira wezeshi.
Aliutaka pia Mkoa wa Morogoro kuongeza kasi katika mpango wa uwekezaji wa viwanda kutokana na mazingira mazuri yaliyopo, ambapo kwa sasa katika Eneo Maalumu la Uwekezaji (EPZ) viwanda vinne vitajengwa na kusaidia kuongeza ajira kwa vijana.
Alisema katika uwekezaji, Mkoa wa Pwani unaongoza na Morogoro unafuatia.
Aliagiza mapato ya halmashauri yatumiwe pia kutenga asilimia 10 kwa vijana na wanawake ili kusaidia vikundi vya uzalishaji mali. Ahutubia Gairo Akiwa wilayani Gairo eneo la Unguu Road, Makamu wa Rais aliambiwa juu ya tatizo kubwa la maji, kwamba mradi mkubwa wa Benki ya Dunia wa thamani ya Sh bilioni sita, haujaweza kumaliza tatizo hilo.
Samia pamoja na hayo, aliridhia ombi la Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk Stephen Kebwe la kuondoka na Meneja wa Wakala wa Misitu wa Wilaya ya Gairo, Adinanani Mrema baada ya kutuhumiwa kutosimamia majukumu yake ya kazi kikamilifu huku misitu ikiteketea, ambapo Makamu wa Rais alisema ataondoka naye ili kuangalia hatua zaidi za kuchukua dhidi yake.
Awasili Dodoma
Safari ya Makamu wa Rais iliishia mjini Dodoma, ambapo aliweza kuwasili jioni kuanza ziara ya siku nne mkoani humo.
Ofisa Habari wa Mkoa huo, Jeremia Mwakyoma akizungumzia ziara ya Samia, alisema leo atatembelea jengo la Mkuu wa Mkoa, linalojengwa na serikali na dampo la Chidaye, lililopo nje kidogo ya mji wa Dodoma.
Baada ya ziara hiyo kwenye dampo, atafanya mkutano na makundi mbalimbali ya wakazi wa mji wa Dodoma, wanaoendesha shughuli zenye mahusiano na masuala ya Mazingira katika ukumbi wa Hazina Ndogo.
Aidha kwa mujibu wa ratiba hiyo, kesho anatarajiwa kufungua Mkutano wa mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Waganga Wafawidhi wa Hospitali za Mikoa Tanzania Bara. Akifafanua, Mwakyoma alisema ziara ya Makamu wa Rais inalenga kukagua shughuli mbalimbali za maandalizi ya kupokea ujio wa Serikali mkoani hapa.
Tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ameshahamia mkoani hapa na ameshafanya ziara kadhaa za kuangalia juhudi za kuufanya mji wa Dodoma, kupokea ujio wa serikali na kuhakikisha mipango miji inakwenda kwa jinsi inavyokusudiwa.
Alitumia ziara zake hizo kwanza, kuwatoa wasiwasi watumishi watakaohamia Dodoma kuwa hakuna shida ya matibabu ya huduma za afya, huduma za jamii kama chakula, maji, umeme na shule.
Aidha aliwataka wafanyabiashara kujipanga kutokana na ujio wa serikali Dodoma, ambapo watumishi 2,700 watahamia Dodoma. Alisema uhamiaji huo utakuwa wa awamu sita.
Habari hii imeandikwa na John Gagarini, Kibaha na Sifa Lubasi, Dodoma.
0 Comments