MKUU wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo ameiagiza Takukuru kufanya uchunguzi dhidi ya mkandarasi Duwi Construction and Engineering Co. Ltd anayetuhumiwa kughushi nyaraka zinazoonesha alijenga barabara ambazo hazimo kwenye orodha ya barabara za mkoa huo.
Aidha, Naibu Waziri wa Kilimo, Chakula na Mifugo, William ole Nasha ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro, ameipongeza serikali kutangaza zabuni hivi karibuni kwa ajili ya ujenzi wa barabara za kiwango cha lami wilayani humo.
Awali, katika kikao cha 38 cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Arusha kilichohudhuriwa na Gambo, Mhandisi wa Barabara Mkoa, Edward Amboka alitoa taarifa za hali ya barabara mkoani hapa, alisema wanamfuatilia mkandarasi huyo anayetuhumiwa kughushi nyaraka na kuidanganya bodi ya manunuzi kuwa amejenga barabara kwenye halmashauri nyingine huku akijua si kweli.
Amboka alisema wanashangaa kwa nini mkandarasi huyo aliomba kazi wilayani Monduli mwaka 2015/16 na mchakato wa kuomba kazi ulifanyika na akapewa fursa ya kuendelea na ujenzi huku wajumbe wa zabuni walipaswa kuhakiki kama kweli ana vigezo vinavyostahili pamoja na vifaa.
Alisema mkandarasi huyo alidaiwa kuwasilisha nyaraka zisizo za kweli, ambapo miongoni mwa nyaraka hizo ni zile zinazohusu kazi alizowahi kuzifanya kwenye halmashauri ya Wilaya ya Arusha kuwa alijenga barabara ya Oldonyosambu - Ngaramtoni, huku akijua barabara hiyo haipo kwenye mtandao wa barabara za mkoa.
Pia alituhumiwa kughushi logo ya mkoa, akitumia namba AR/RR, badala ya ile inayotambulika mkoani kwa wahusika wa barabara za mkoa, inayoanzia na kumbukumbu namba LGA na kuwasilisha kwenye bodi kazi nyingine, alizowahi kufanya kama kujenga barabara ya Nkoarua-Sing'isi ambayo haipo kwenye mtandao wa barabara kimkoa.
Pia alituhumiwa kughushi saini ya Mhandisi, Gibson Kisanga ambaye awali alikuwa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha na mwaka 2013, alihamishiwa wilayani Longido.
Pia aliomba tena kujenga barabara ya Endabashi - Manyara hadi Basuda wilayani Karatu kwa gharama ya Sh milioni 141.1 kwa mwaka 2015/16 na hadi sasa, anaendelea na kazi hiyo kwa kusuasua.
Baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, Gambo alihoji waliohusika kumpa zabuni mkandarasi asiye na sifa na kutoa amri kwa Takukuru kuchunguza waliotoa zabuni hiyo.
Wajumbe wa kikao hicho walipendekeza kuwa, baadhi ya barabara katika kila wilaya zinatakiwa kupandishwa hadhi na kuingizwa kwenye orodha ya Tanroads, Arusha kwa ajili ya kujengwa barabara kwa viwango vya lami au changarawe ili kupitika kwa urahisi.
Ole Nasha ambaye ni Mbunge wa Ngorongoro, alimshukuru Gambo kuwezesha mkoa huo kupata maendeleo, kwani miaka kadhaa iliyopita wilaya hiyo, yenye maajabu saba ya dunia, baadhi ya barabara zake zilikuwa hazina lami, lakini sasa zitakuwa na lami.
|
0 Comments