Johnson Nguza aka Papii Kocha akitumbuiza kwa pamoja na wanamuziki wa Twanga Pepeta wakati wa Tamasha la Michezo katika kuadhimisha siku ya Nyerere Nchini lililofanyika gerezani Ukonga jijini Dar es salaam, tarehe 14.10.2016.
Na ASP Deodatus Kazinja wa Jeshi la Magereza.
Katika kuadhimisha miaka 17 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere Gereza Kuu Ukonga kwa kushirikiana na Kampuni ya Global Publishers limefanya Tamasha la michezo mbalimbali kwa wafungwa wa gereza hilo.
Akiongea katika Tamasha hilo Mkurugenzi wa Global Publishers aliyekuwa pia mgeni rasmi Bwana Eric Shigongo amewaambia wafungwa kuwa dhimra ya ujio wao gereza ni katika kuonesha kuwathamini, kuwahurumia na kuwatia moyo kwamba kuwa kwao gerezani siyo kwamba wametengwa na dunia.
Bwana Shigongo aliwatia moyo wafungwa hao kuwa hawatakiwi kukata tamaa na bado wanayo nafasi ya kubadilika na kuwa raia wema. “Kila mwanadamu anaowajibu wa kubadili maisha yake, Mwalimu Nyerere tunayemuadhimisha leo alizaliwa kama mimi na wewe na kutengeneza maisha yake na leo tunamkubuka kwanini wewe ushindwe?”
Aliongeza “ najua wengi wenu mko hapa mkiwa mmeitwa majina mengi kwakuwa mmehukumiwa, hizini hukumu za wanadamu, mnaouwezo wa kuandika kurasa mpya katika maisha yenu na siku mkitoka duniani waseme mtu mwema ameondoka. Siku moja inatosha kubadili maisha yako, kila siku andika ukurasa mpya wa maisha yako na Mungu atakuongoza alisisitiza Shigongo.
Wadau wengine walioungana na Global Publishers katika tukio hilo ni pamoja na Tume ya Haki za Binadamu Nchini ikiongozwa na mwenyekiti wake Thom Nyanduga na ndugu Rajab Maranda (aliyewahi kuwa mfungwa gereza Ukonga) ambao kwa pamoja walileta zawadi mbalimbali kwa wafungwa hao ikiwemo vifaa vya, sabuni,soda kikombe ambacho kilitolewa kwa timu iliyofanya vizuri katika mpira wa miguu.
Katika Tamasha hilo wafungwa walishiriki michezo ya kukimbia katika magunia, kukimbia na yai katika kijiti, mbio za mita 100 vijana kwa wazee, mita 400 kupokezana vijiti, kuvuta kamba, mieleka, mpira wa miguu, mashairi, kuonesha vipaji vya uchekeshaji, kuimba kwa mtindo kufokafoka, ngoma za jadi na burudani kwa kushirikiana na baadhi ya wanamuziki wa bendi ya Twanga pepeta.
Picha zote na Deodatus Kazinja wa Jeshi la Magereza.
0 Comments