TEMBO wanaotoka katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti wameendelea kuleta kero kwa wananchi wa vijiji vya Wilaya ya Bunda mkoani Mara, vinavyopakana na hifadhi hiyo.
Tembo hao wanaleta fujo kwa kushambulia mazao yao shambani na kwenye maghala, hali inayohatarisha maisha yao kutokana na wanyama hao kuingia hadi kwenye makazi ya watu.
Mwanzoni mwa wiki, wanyama hao walivamia makazi ya wananchi na kushambulia mazao kikiwamo chakula kilichohifadhiwa kwenye maghala pamoja na kushambulia shamba kubwa la katani la mwekezaji katika kata ya Nyatwali wilayani hapa.
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Charles Mlingwa alitembelea maeneo ambayo wanyama hao wameleta hasara kubwa na kushuhudia uharibifu huo.
Mkuu wa Mkoa huyo, alifanya mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kunzungu na wananchi kutoka kata za Kunzugu, Balili, Bunda Stoo, Nyatwali walishiriki na akatoa fursa kutoa kero zao, walisema wanyama hao wamekuwa wakishambulia vyakula shambani na kwenye maghala hivyo wanakabiliwa na njaa.
“Tunashukuru kwa kuja, lakini kutokana na wanyama kuvamia na kushambulia vyakula vyetu, tuna njaa.....tunaomba chakula cha msaada,” alisema Joseph Paul.
Akijibu kero hizo, Dk Mlingwa aliwapa pole wananchi hao na kusema kuwa ni kweli wanyama hao wameleta hasara kubwa kwa wakazi hao.
Alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Janeth Mayanja, kufanya tathmini haraka ili kujua hasara iliyosababishwa na wanyama hao.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mji wa Bunda, Mayanja aliiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kuchukua hatua madhubuti kuwadhibiti wanyama hao kwa kuwa takwimu zinaonesha wanavamia vijiji vya jirani hasa upande wa kusini mwa hifadhi hiyo, na tatizo lilianza kutokea mwaka 2012.
|
0 Comments