Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Oct 31, 2016

Viagra kiini cha kuua kakakuona

MATUMIZI ya dawa za kuongeza nguvu za kiume, lishe na mapambo katika majumba ya kifahari, imeelezwa kuwa ni kichocheo kikubwa cha kushamiri kwa biashara ya wanyama adimu kakakuona barani Asia, hususani nchini China na Vietnam.
Hatua hiyo inachangiwa kuwindwa kwa wanyama hao kila kona na ni baada ya nchi za Asia wanyama hao kutoweka ambapo kwa sasa usakaji wake umehamia barani Afrika na hasa katika nchi za kusini mwa jangwa la Sahara na Afrika Mashariki na Kati.

Ofisa Maliasili wa Mkoa wa Morogoro, Joseph Chuwa alisema hayo juzi mjini hapa baada ya kukamatwa kwa mifuko 67 ya magamba ya kakakuona. Kwa mujibu wa Chuwa, biashara hiyo imekuwa ikifanyika katika nchi za Afrika Mashariki na Kati ambako soko lake kubwa ni katika nchi za Bara la Asia hasa China na Vietnam.
Alisema magamba ya mnyama huyo inashabiahana na vitu vilivyomo ndani ya pembe ya faru ambavyo baadhi ya watu katika nchi hicho wanasaga magamba hayo na kuwa unga ambao unadaiwa kuwa ni dawa ya kuongeza nguvu za kiume.
Hivyo alisema kutoweka kwa wanyama hao katika nchi hizo na mabara mengine kunawafanya maharamia hao kusaka barani Afrika na sasa ikiwemo Tanzania.
Alisema pamoja na wanyama hao kutumiwa kama vitoweo katika nchi za mabara hayo, pia magamba yake husagwa kuwa unga ambao hutengenezwa dawa zinazoongeza nguvu za kiume pamoja na mapambo katika majumba makubwa ya kifahari.
Hivyo, alisema kakakuona ni miongoni mwa wanyama wanaolindwa na Jumuiya ya Kimataifa ya kuhifadhi wanyama walio katika hatari ya kutoweka duniani.
Chuwa aliwaomba wananchi wa Mkoa wa Morogoro kushirikiana na serikali na vyombo vya dola ili kuwafichua wahalifu wanaoangamiza wanyamapori wakiwemo kakakuona ambao ni adimu kupatikana ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
Alisema kukamatwa kwa watuhumiwa hao watavisaidia vyombo vya dola kubaini mtandao wa biashara hiyo na kukomesha kuuawa kwa kakakuona ambao ni wachache.
Polisi mkoani Morogoro imewakamata watu wanne wakiwemo raia watatu wa kutoka Burundi baada ya kukutwa na magamba ya mnyama adimu kakakuona yakiwa yamehifadhiwa katika mifuko 67, ambayo thamani yake ni zaidi ya Sh bilioni 1.4 na yakisubiri kusafirishwa kwenda masoko ya nje ya nchi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema watu hao walikamatwa saa tano na nusu usiku wa Oktoba 28, mwaka huu eneo la mtaa wa Reli, Kata ya Kichangani, Manispaa ya Morogoro ndani ya ghala moja lenye mashine ya kukoboa na kusaga nafaka.
Kamanda Matei aliwataja raia watatu kutoka Burundi waliokamatwa ni Kibonese Golagoza (35), Nuru Athuman (32) na Benjamin Luvunduka (41) ambao pia ni wakazi wa Morogoro, wakati Mtanzania aliyekamatwa ni Shukuru Mwakalebela (25) mkazi wa Stesheni mjini Morogoro.
Kwa mujibu wa Kamanda Matei, watuhumiwa hao walikamatwa na magamba ya kakakuona mifuko 67 ikiwa imehifadhiwa katika mifuko ya kilo 50 na kisha kutumbukiza kwenye viroba vya kilo 100 ambavyo vilivyochanganywa na maharage.
Chuwa aliyekuwepo katika ukamataji huo, alisema katika mifuko 67 iliyokamatwa kila mmoja ulikuwa na wastani wa magamba ya kakakuona 1,000.
Alisema kakakuona mmoja kwa wastani anakuwa na magamba 60 hadi 100, hali iliyofahamika kuwa kila mfuko mmoja wenye kuhifadhi magamba hayo ni sawa na kakakuona wapatao 10 waliouawa kwa ajili ya biashara hiyo haramu.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP