KAMATI za Kudumu za Bunge zimemaliza rasmi vikao vyake mwishoni mwa wiki huku vikionesha makali yake katika kuzisimamia na kudhibiti hasa matumizi ya hesabu kwa taasisi mbalimbali za serikali.
Kamati hizo zilizoanza vikao vyake tangu Oktoba 16, mwaka huu mjini hapa zilikutana na wizara na taasisi mbalimbali na kupitia, kujadili na kuboresha mipango ya taasisi hizo za serikali, ikiwa ni moja wa wajibu wa kazi za Bunge.

Katika kipindi hicho, mawaziri, wakurugenzi, makatibu wakuu na wenyeviti wa bodi waliwasilisha taarifa za utendaji na hesabu za taasisi zao mbele ya kamati hizo, ikiwa ni pamoja na kujibu hoja mbalimbali zilizoibuliwa katika taarifa ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka unaoishia Juni, 2015.
Katika vikao hivyo, hoja mbalimbali ziliibuliwa, ikiwa ni pamoja na taarifa mbalimbali kukataliwa kutokana na kubainika kuwa na upungufu tofauti na matakwa ya kamati hizo kwa mujibu wa sheria.
Kamati ya mbalimbali, ikiwemo Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) ililazimika kugomea kujadili taarifa zilizowasilishwa mbele yake huku zikitoa kauli na maagizo makali dhidi ya taasisi husika. Moja ya taasisi iliyorejeshwa na kutakiwa kurejea mbele ya PAC kutokana na upungufu uliobainika ni Mfuko wa Pensheni wa PSPF ambao ulifika mbele ya kamati hiyo bila upande wa serikali kuwepo.
Hata hivyo, siku mbili baadaye shirika hilo lilifika mbele ya kamati hiyo likiambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Dorothy Mwanyika ambaye alijibu hoja za taasisi hiyo kwa niaba ya serikali. Hoja kubwa iliyoibuliwa katika kikao hicho ni hali ya mbaya ya kifedha ya PSPF kwa mujibu wa ripoti ya CAG inayoishia Juni, 2015 inayoonesha kuwa taasisi hiyo inatengeneza hasara ya zaidi ya Sh trilioni 11.15.
Pamoja na kamati hiyo, makali mengine yalioneshwa na Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) katika kupitia taarifa ya hesabu za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam kwa mwaka unaoishia Juni, 2015 eneo la Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA).
Kamati hiyo ililazimika kuutimua uongozi wa Jiji hadi pale utakapofika mbele ya kamati hiyo ukiwa umeambatana na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mwanasheria Mkuu na Msajili wa Hazina ili kutoa majibu ya uhakika kuhusu kuuzwa kwa hisa za shirika hilo.
Waziri George Simbachawene, AG George Masaju na Msajili Lawrence Mafuru walifika mbele ya kamati hiyo kama ilivyoagiza ambako pamoja na kutoa ufafanuzi, walianika hadharani wamiliki halali wa Kampuni ya Simon Group inayodaiwa kuuziwa kinyemela hisa za UDA. Taasisi nyingine iliyoonja joto la Kamati za Kudumu za Bunge ni Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) ambalo lilitimuliwa kwenye kikao cha PAC.
Shirika hilo lilikutwa na dhahama hiyo kutokana na kukiuka kanuni za Bunge kwa kushindwa kuwasilisha kwa wakati nyaraka ya taarifa za shirika hilo kuhusu hesabu zake zinazoishia Juni mwaka 2015. Wajumbe wa PAC waligoma kuijadili taarifa yao na kudai kuwa mhimili wa Bunge umedharauliwa kwa kuwa taarifa hiyo iliwasilishwa asubuhi siku ya kikao badala ya siku tatu kabla kwa mujibu wa kanuni za Bunge.
Mbunge wa Malinyi, Hadji Mponda alisema hiyo si mara ya kwanza kwa shirika hilo kukiuka maagizo na kanuni za Bunge, kwani hata mwaka juzi walikaidi kuwasilisha taarifa za mikataba ya gesi mbele ya kamati hiyo ya PAC, hali iliyosababisha viongozi wake kuburuzwa Polisi na kushtakiwa.
Mawaziri wengine waliofika na kutoa majibu ya hoja kuhusu wizara na taasisi zilizo chini ya wizara zao ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk Medard Kalemani na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage.
Wengine ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Aidha, katika kamati hizo, pia wenyeviti wa bodi na wakurugenzi wakuu wa mashirika mbalimbali waliwasilisha na kujibu hoja kuhusu taasisi zao mbele ya kamati hizo ambao ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Tanzania Standard Newspapers inayochapisha magazeti ya HabariLeo, Daily News na SpotiLeo, Dk Jim Yonazi.
Wengine ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu, Kaimu Kamishna wa Nishati na Petroli, James Andilile, Mkurugenzi wa NSSF, Profesa Godius Kahyarara na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme (Tanesco), Felchesmi Mramba, Katibu Mkuu wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhem Meru, viongozi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA), uongozi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.
Baadhi ya wabunge waliozungumza na gazeti hili kuhusu wajibu wa kamati hizo, walibainisha wazi kuwa kazi ya kamati ni kuisimamia serikali na kuhakikisha inatimiza wajibu wake katika kuwahudumia Watanzania kupitia sekta mbalimbali. Mbunge wa Vwawa, Joseph Hasunga alisema kazi kubwa ya Kamati za Bunge ni kuisimamia na kuishauri serikali juu ya namna ya kuboresha huduma zake kwa jamii, hivyo lazima, kamati hizo zitimize wajibu wake kwa kuhakikisha zinaheshimiwa.
“Kamati za Bunge ni sawa na Bunge, unapoidharau au kuidanganya umelidanganya Bunge, ndio maana inabidi tuwe wakali ili na sisi tuweze kutimiza wajibu wetu,” alisema Hasunga anayetoka Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Viwanda na Biashara na Mbunge wa Igunga, Dk Dalaly Kafumu alisisitiza kuwa kazi kubwa ya kamati si kusimamia na kujadili tu taarifa za serikali au taasisi za serikali, bali pamoja na kufanya ukaguzi wa miradi ya serikali ili kuhakikisha utendaji wake. Baada ya kumalizika kwa vikao vya Kamati hizo za Kudumu za Bunge, Bunge la 11 kesho litaanza Mkutano wake wa Nne.