MGOGORO wa Chama cha Wananchi (CUF) umechukua sura mpya baada ya Bodi ya Baraza la Wadhamini wa chama hicho kwenda mahakamani, kuomba kibali cha kufungua kesi dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi.
Mbali ya Mutungi, bodi hiyo inaomba kufungua kesi dhidi ya Mwenyekiti wa Taifa wa CUF, aliyejiuzulu, Profesa Ibrahim Lipumba na wanachama 12 wa chama hicho ambao walisimamishwa.

Bodi hiyo iliwasilisha maombi hayo jana mchana katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kupitia kwa Wakili wa chama hicho, Juma Nassoro na kusajiliwa kwa namba 75 ya mwaka 2016.
Hatua ya bodi kukimbilia mahakamani inatokana na mgogoro unaoendelea ndani ya chama hicho, baada ya Profesa Lipumba aliyejiuzulu Uenyekiti Agosti 6, mwaka huu, kutangaza kurejea kwenye wadhifa huo kwasababu Jaji Mutungi alitoa kauli kuwa Lipumba bado ni Mwenyekiti halali wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kesi hiyo, Wakili Nassoro alisema wamefungua maombi hayo ya kutaka kufungua kesi hiyo na kuiomba Mahakama itoe amri ya kutaka Jaji Mutungi asijihusishe na masuala ya kisiasa nje ya Mamlaka, Kanuni na taratibu za Sheria ya Vyama vya Siasa.
Alisema wanaomba mahakama iwape kibali cha kupata amri ya mahakama kumzuia msajili asijihusishe na masuala ya kisiasa nje ya mamlaka aliyopewa na Kanuni pamoja na Sheria ya vyama vya siasa.
“Tunafahamu mahakama ilishawahi kutoa amri inayotoa tafsiri ya mamlaka ya msajili lakini saizi tunataka mahakama iende mbali zaidi imzuie msajili aifanye kazi kinyume na mamlaka aliyopewa,” alisema Nassoro.
Aliongeza kuwa bodi iliyofika mahakamani hapo kuwasilisha maombi ya kutaka kufungua kesi, ndiyo inayotambulika kisheria, hivyo hakuna bodi mbili ndani ya CUF.