Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametatilisha hukumu ya wafungwa zaidi ya elfu mbili ambao walikuwa wamehukumiwa kifo.
Rais amebadilisha hukumu hiyo na sasa wafungwa hao 2,747 watatumikia hukumu ya maisha jela.

Wahalifu wamekuwa wakihukumiwa kifo Kenya lakini hakuna aliyewahi kuuawa tangu miaka ya 1980.
Watetezi wa haki wamekuwa wakipigania kuondolewa kwa hukumu hiyo.
Baadhi ya wafungwa hata hivyo wamekuwa wakilalamika kwamba hakuna tofauti ya hukumu ya kifo na maisha jela kwani mfungwa huwa anaishi jela hadi kifo chake.
Rais Kenyatta pia amewaachilia huru wafungwa 102 waliokuwa wakitumikia vifungo virefu.
Alhamisi wiki iliyopita, Rais Kenyatta alikuwa amewaachilia huru wafungwa takriban 7,000 wa makosa madogo madogo au waliokuwa wanakaribia kumaliza kutumikia vifungo vyao, na ambao walikuwa wameonyesha dalili za kubadilisha tabia.