Askofu Dk Owdenburg Mdegella
MWENYEKITI wa Bodi ya Chuo Kikuu cha Iringa (UoI), Askofu Dk Owdenburg Mdegella amepongeza uamuzi wa Serikali ya Awamu ya Tano ya uhakiki wa vyeti vya watumishi wake, akisema utasaidia kumaliza hali mbaya ya ongezeko la vyeti bandia.
Akizungumza kwenye mahafali ya 19 ya chuo hicho juzi, Askofu Dk Mdegella alisema uhakiki huo una mafanikio, kwani unapembua chuya kutoka kwenye mchele safi.

“Kwa kupembua chuya, serikali inataka kubaki na wajuzi wenye vyeti halali katika utumishi wake wa umma, jambo linalopaswa kupongezwa,” alisema Dk Mdegella.
Alisema katika mizania ya utoaji wa ajira haikuwa sahihi yule aliyekaa darasani kwa miaka mitatu akawa na fursa sawa au wakati mwingine kuzidiwa na aliyepata cheti kutoka Kariakoo (Dar es Salaam) tena kikiwa na ufaulu wa juu.
“Watu hawa wanaweza kuwa na haki na maslahi yanayofanana, lakini tofauti yao ni kwamba yule aliyepata vyeti bandia vyenye ufaulu wa hali ya juu anakuwa hana ujuzi wa kazi aliyopewa, jambo lililokuwa likirudisha nyuma maendeleo ya taasisi nyingi na nchi kwa ujumla,” alisema.
Alisema uhakiki wa vyeti unapaswa kuungwa mkono na wadau wote na kuna haja usiishie kwa watumishi wa umma, bali uende hadi kwa watumishi wa sekta binafsi.
Akizungumzia maendeleo ya chuo hicho ambacho zamani kilijulikana kama Chuo Kikuu cha Tumaini, Kampasi ya Iringa, Dk Mdegella alisema kinajipanga kuachana na mtazamo wa muda mrefu wa kujiendesha kwa kutegemea wafadhili mbalimbali wa ndani na nje ya nchi pamoja na mikopo ya ada za wanafunzi kutoka serikalini.
Ili kufikia lengo hilo, alisema wanatarajia kuanzisha asasi itakayounganishwa na chuo hicho ambayo kazi yake kubwa itakuwa kutoa mikopo kwa wanafunzi wanaokosa huduma hiyo kutoka serikalini na maeneo mengine.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Joseph Madumula alisema mazingira ya utoaji wa elimu kwa sasa yamekuwa na ushindani mkubwa tofauti na miaka ya nyuma, hali hiyo ikichangiwa na ongezeko la vyuo vikuu katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema wamejipanga kutoa elimu shirikishi ya ujasiriamali kwa wanafunzi wote wa chuo hicho ili wakimaliza wasitegemee kuajiriwa tu, bali wawe na uwezo wa kujiajiri na kuzalisha ajira kwa vijana wengine.
Mkuu wa chuo hicho, Jaji Mkuu mstaafu Agustino Ramadhani alisema ni vema wahitimu wakawa wazalendo kwa nchi yao na kuitumia elimu wanayopata kwa maendeleo ya Watanzania wote.