Rais John Magufuli
RAIS John Magufuli ambaye wakati anaingia madarakani mwaka mmoja uliopita, alieleza kuwa moja ya kazi kubwa ya serikali yake itakuwa ni kukusanya kodi, ameifumua Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kuvunja Bodi ya Wakurugenzi na kuteua Naibu Kamishna Mkuu mpya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa jana, Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TRA, Bernard Mchomvu na kuivunja Bodi nzima.

Aidha, pamoja na kuivunja bodi hiyo amemteua Charles Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, kuziba nafasi iliyokuwa wazi kwa mwaka mmoja baada ya Dk Magufuli kutengua uteuzi wa aliyekuwa akishikilia wadhifa huo, Lusekelo Mwaseba.
“Uteuzi wa Mwenyekiti mwingine wa Bodi ya Wakurugenzi wa TRA na Bodi ya Mamlaka hiyo utatangazwa baadaye,” ilieleza taarifa ya Ikulu jana asubuhi.
Saa chache baada ya kuvunja bodi hiyo, Dk Magufuli alitangaza uteuzi wa Kichere kuwa Naibu Kamishna Mkuu wa TRA. Kwa mujibu wa Ikulu, Kichere anajaza nafasi iliyokuwa wazi kwa zaidi ya mwaka mmoja.
“Uteuzi huo umeanza mara moja,” ilieleza taarifa hiyo. Bodi ya Wakurugenzi iliyokuwa ikiongozwa na Mwenyekiti Mchomvu ilikuwa na wajumbe 11 na ilipaswa kumaliza muda wake mwakani, ikianza kazi mwaka 2014.
Kwa mujibu wa shajara ya mwaka huu ya TRA, wajumbe wa bodi hiyo ambayo waliteuliwa mwaka 2014 na walitakiwa kuhudumu hadi mwaka 2017 na maeneo waliyokuwa wakifanya kazi wakati wakiteuliwa kwenye mabano ni Shogholo Msangi (Kamishna Msaidizi wa Sera, Wizara ya Fedha), Khamis Omari (Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Zanzibar) na Dk Philip Mpango (akiwa Katibu Mkuu Tume ya Mipango). Kwa sasa, Dk Mpango sasa ni Waziri wa Fedha na Mipango.
Wengine ni Profesa Beno Ndullu (Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania-BoT), Assaa Ahmad Rashid (Katibu Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar), Josephat Kandege (Mbunge Kalambo – Rukwa), Dk John Mduma (Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Utafiti wa Uchumi na Sera Chuo Kikuu cha Dar es Salaam -Udsm), Dk Nsubili Isaga, (Mhadhiri Chuo Kikuu cha Mzumbe), na Rished Bade (akiwa Kamishna Mkuu TRA). Katibu wa Bodi hiyo alikuwa Juma Beleko (TRA).
Taarifa ya Ikulu haikueleza sababu za kutengua uteuzi wa Mchomvu aliyewahi kuwa Katibu Mkuu na baadaye Ofisa Mtendaji Mkuu wa Akaunti ya Changamoto za Milenia (MCA), lakini kutokana na msimamo wa Rais Magufuli katika masuala ya kodi hasa ukusanyaji wake, bila ya shaka hajaridhishwa na utendaji wa bodi hiyo.