MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Nkasi katika Mkoa wa Rukwa, imemhukumu mwendesha pikipiki maarufu ‘bodaboda' Said Mshani (18) maarufu kama “Mbalizi” kutumikia kifungo cha miaka miwili jela na kulipa faini ya Sh 500,000, baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la kufanya shambulio la aibu kwa abiria wake wa kike.

Akisoma hukumu hiyo juzi, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Lilian Lutahangwa alisema kuwa, upande wa mashitaka umetoa ushahidi wake pasipo kutia shaka yoyote kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo.
Awali Mwendesha Mashitaka, Mkaguzi wa Polisi, Hamimu Gwelo alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari , 21 mwaka huu saa saba usiku katika Mji wa Namanyere.
Ilidaiwa kuwa usiku wa tukio, mshitakiwa akiwa katika stendi ya zamani mjini Namanyere, alifika abiria wa kike ambapo alimueleza ampeleke nyumbani kwake katika kitongoji cha Mabatini.
Mwendesha Mashitaka, Gwelo alidai kuwa mwendesha bodaboda akiendesha aliiangusha pikipiki kwa makusudi, wakati abiria wake akiwa anagaragara chini alianza kupapasa mwili bila ridhaa yake huku akimshika matiti, makalio na sehemu za siri.
Gwelo aliongeza kuwa, mshitakiwa alichana sketi ya abiria wake, na kumuacha akiwa na nguo yake ya ndani.
Akijitetea, mshtakiwa huyo ambaye ni mkazi wa kitongoji cha Kipundukala kilichopo katika Mji wa Namanyere, alisisitiza hakutenda kosa hilo.