Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ametoa mwito huo jana wakati anajibu ujumbe  ulioelekezwa kwake na wananchi kwa njia ya mabango, wakitaka kupata kauli ya serikali kuhusu tatizo la njaa.
Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo, Estomiah Chang’ah alisema, tatizo la upungufu wa chakula limesababishwa na ukame ulioingilia msimu wa kilimo hasa muhogo ambao ni chakula kikuu, umeshambuliwa na magonjwa ya batobato na michirizi kahawia.

Mama Samia alisema, wakati serikali ikiendelea kufanya tathmini ya tatizo hilo, ni vyema wananchi wakatafuta njia mbadala ya kukabili tatizo hilo kwa kulima mazao yanayokomaa kwa muda mfupi kama viazi vitamu.
Akisisitiza Makamu wa Rais, Samia aliwataka wananchi kuacha kusubiri chakula cha msaada, kwa sababu hakitatolewa bure na akarudia kauli ya Rais John Magufuli kuwa asiyefanya kazi na asile.
Wakati huo huo, aliaugiza uongozi wa mkoa wa Mwanza kufuatilia na kuhakikisha miradi ya kilimo cha umwagiliaji katika vijiji vya Bugorola na Muyogyezi vilivyoko wilayani Ukerewe, inakamilika.
Alisema miradi hiyo ikikamilika, itasaidia kuzalisha chakula cha kutosha kwa muda wote, na hivyo kupunguza tatizo la upungufu wa chakula, unaosababishwa na hali mbaya ya hewa kama ukosefu wa mvua.
Hata hivyo alipongeza juhudi zinazofanywa na halmashauri hiyo, ikiwamo ya ujenzi wa kituo cha Polisi katika kisiwa cha Ghana, kuongeza mapato ya ushuru hadi asilimia 90 na kutekeleza utaratibu wa kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka.