Francois Fillon ndiye atakayekuwa mgombea urais wa chama cha wahafidhina nchini Ufaransa baada ya mpinzani wake Alain Juppe kukubali kushindwa.
Baada ya kura nyingi kuhesabiwa, bw Fillon alikuwa anaongoza akiwa na karibu asilimia 67 ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi wa mchujo Jumapili.
Bw Fillon ameahidi kuunda jamii yenye usawa na haki zaidi, akisema Ufaransa inahitaji "ukweli an inahitaji hatua zichukuliwe".
Sasa huenda akakabiliana na mgombea wa chama cha Kisosholisti na mgombea wa chama cha mrengo wa kulia Marine Le Pen uchaguzini mwezi Aprili.
Bw Juppe, ambaye siasa zake sana ziliegemea msimamo wa wastani, alimpongeza Bw Fillon kwa ushindi wake "mkubwa" na akaahidi kumuunga mkono katika juhudi zake za kutana kuwa rais.
Baada ya kura kutoka vituo 9,713 kati ya 10,229 kuhesabiwa, Fillon alikuwa ameshinda 66.6% naye Bw Juppe 33.4%.

Alain JuppeImage copyrightREUTERS
Image captionAlain Juppe ni waziri mkuu wa zamani na meya wa sasa wa Bordeaux

Bw Fillon alitarajiwa kushinda mchujo baada ya kupata asilimia 44 ya kura kwenye awamu ya kwanza ya mchujo wiki moja iliyopita ambapo rais wa zamani Nicolas Sarkozy alitupwa nje.
Bw Fillon, ambaye alikuwa waziri mkuu katika serikali ya Bw Sarkozy, 62, ni Mkatoliki alitazamwa kama mwenye kuegemea msimamo wa kitamaduni katika masuala kama vile utoaji mimba na ndoa za wapenzi wa jinsia moja.
Anapendekeza mageuzi makubwa ya kiuchumi ikiwemo kupunguza nafasi za kazi serikalini 500,000 na kumaliza mpango wa kufanya kazi kwa saa 35 kwa wiki, kuongeza umri wa kustaafu na kuondoa ushuru unaotozwa utajiri.
Macho sasa yaanelekezwa kwa chama cha Kishosholisti, kuona iwapo Rais Francois Hollande ambaye amepoteza umaarufu, atawania tena na kushiriki mchujo wa chama hicho Januari.
Anatarajiwa kutangaza uamuzi wake siku chache zijazo.
Waziri Mkuu Manuel Valls alisema Jumapili kwamba hajafutilia mbali uamuzi wa kuwania dhidi ya Bw Holland kwenye mchujo.
Emmanuel Macron, 38, waziri wa zamani wa uchumi na mwanafunzi wa kisiasa wa Bw Hollande tayari ametangaza atawania kama mgombea huru wa kuegemea mrengo wa kati.