Mwandishi wa wahabari wa runinga ya KTN kutoka Kenya Joy Doreen Biira alikamatwa na kuzuiliwa na maafisa wa usalama nchini Uganda usiku wa Jumapili.
Vyombo vya habari zinasema Bi Biira alikamatwa pamoja na wengine watano kwa tuhuma za kupiga picha na video kuhusu operesheni ya maafisa wa usalama katika kasri la mfalme wa Rwenzururu na kuzichapisha kwenye mitandao ya kijamii.

Wanahabari na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu wametoa wito kwa serikali kumwachilia huru.
Kitambulisha mada #FreeJoyDoreen (Mwachilie huru Doreen) kinavuma katika mtandao wa Twitter nchini Kenya.
Wanajeshi na polisi walivamia kasri hilo la Mfalme Charles Wesley Mumbere Jumapili.
Walinzi wake 46 waliuawa kwa mujibu wa polisi, na wengine 139 wakakamatwa.
Mfalme huyo alikamatwa pia na kuzuiliwa makao makuu ya polisi ya wilaya ya Kasese kabla ya kuhamishiwa mjini Kampala.
Gazeti la kibinafsi ya Monitor nchini humo linasema mfalme huyo anatarajiwa kukutana na Rais Yoweri Museveni baadaye leo.