Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

Aidha imezitaka halmashauri hizo kutumia mifumo ya kielektroniki katika ukusanyaji wa mapato na katika maeneo ya kutolea huduma za afya ili kudhibiti upotevu wa mapato na kuongeza makusanyo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema hayo kupitia hotuba yake ya kuahirisha Bunge, ambayo haikusomwa bungeni na badala yake alitoa hoja ya kuahirisha kutokana na kifo cha ghafla cha Mbunge wa Dimani, Hafidh Ali Tahir (CCM) aliyefariki akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

Majaliwa alisema ili kufikia azma hiyo, uwekwe utaratibu madhubuti wa ukaguzi wa mapato na matumizi ya fedha hizo kwa kushirikiana na wakaguzi wa ndani wa halmashauri.
Alizitaka pia Mamlaka za Serikali za Mitaa kuimarisha mifumo ya udhibiti wa ndani na kuhakikisha thamani ya fedha inapatikana katika kila huduma au bidhaa inayonunuliwa na halmashauri, na kwamba hazina budi kuepuka matumizi ya fedha yasiyo na tija katika shughuli za uendeshaji wake.
Alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 halmashauri ziliidhinishiwa kukusanya mapato ya shilingi bilioni 665.4 na hadi kufikia Septemba zimekusanya shilingi bilioni 114.46 sawa na asilimia 17.2 ya makisio.
“Kiwango hiki cha ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hakiridhishi. Hivyo, naomba nitumie fursa hii kuhimiza halmashauri zote nchini kuongeza jitihada katika kukusanya mapato ya vyanzo vya ndani,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu alisema michango ya wabunge kuhusu taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na taarifa za Kamati za Kudumu za Bunge za Mashirika ya Umma (PAC) na Serikali za Mitaa (LAAC), Serikali imeipokea na itafanyia kazi.
“Kwa kuzingatia ushauri mzuri na mapendekezo yaliyotolewa na Kamati ya LAAC kuhusu ukaguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa mwaka 2013/2014 na 2014/2015, Serikali imeshatoa maelekezo kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha kuwa zinatekeleza kwa ukamilifu maelekezo yote ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa na Kamati nyingine ili kuondoa hoja zilizojitokeza katika taarifa ya CAG,” alisema.