Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki.
KAYA 42,035 zimeondolewa katika Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania zikiwemo kaya hewa 11,212 kutokana na uhakiki uliofanyika kuanzia Februari hadi Oktoba mwaka huu ili kuziondoa kaya ambazo hazina sifa.
Kwa mujibu wa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki, kati ya hao, waliokufa ni kaya 10,424, viongozi 3,745 waliohama sehemu ambapo mpango huo haujaanza 5,267 na wasiokuwa na sifa 11,387.

Waziri Kairuki alitoa takwimu hizo jana wakati akifungua kikao cha kazi kilichohudhuriwa na wakuu wa mikoa, wilaya, makatibu tawala wa mikoa na wilaya na wakurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutoka mikoa wa Rukwa na Katavi kilichofanyika jana mjini Sumbawanga mkoani Rukwa.
Alisema katika uhakiki huo kaya 866 zikiwemo kaya hewa 195 zimeondolewa katika mpango huo katika mikoa ya Rukwa na Katavi. Kwa wastani kaya moja hulipwa kati ya Sh 20,000 hadi 60,000 kwa kutegemea idadi ya watu katika kaya.
Aidha, Kairuki ameagiza watumishi wote waliosababisha matumizi mabaya ya fedha kwa kuwaingiza walengwa wasiostahiki katika mpango huo unaosimamiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) Awamu ya Tatu wachukuliwe hatua za kinidhamu na kijinai kwa lengo la kukomesha tabia hizo.
“Kwa watumishi wa mpango ambao wamesababisha matumizi mabaya ya fedha za mpango huo au waliowaingiza kwenye mpango wanufaika wasiostahili, tumeagiza hatua zilizochukuliwa dhidi yao zifahamike kwa lengo la kukomesha tabia hiyo,” alisisitiza.
“Naomba nisisitize uhakiki wa kaya zilizopo kwenye mpango ni endelevu ni lazima kusimamia utaratibu wa kutoa taarifa kwa wanufaika ambao wamekufa au wamehama ili fedha za serikali zisipotee ovyo nje ya malengo yaliyokusudiwa,” alibainisha.
Kwa upande kwake, Mkurugenzi Mtendaji wa Tasaf, Ladislaus Mwamanga alisema ameagiza uhakiki ufanyike tena mijini ili kuwabaini walengwa zaidi wasiostahiki huku akikiri kuwepo kwa baadhi ya watendaji mpango huo ambao si waaminifu.