Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi
KIAMA cha walioghushi vyeti ama kutumia vyeti vya watu wengine kwa lengo la kujitafutia ajira serikalini, kinakaribia baada ya Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), kubainisha kuwa liko katika hatua za mwisho za kukamilisha uhakiki wa vyeti vya watumishi hao.
Kwa mujibu wa Sheria ya Ajira na Mahusiano ya mwaka 2004, ni kosa la jinai kughushi vyeti.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Ofisa Habari wa Necta, John Nchimbi, alisema mpaka sasa maofisa wa baraza hilo waliosambazwa mikoani kufanya uhakiki huo, wengi wao wamerejea na wachache waliobaki wanakamilisha kazi hiyo ili warejee Dar es Salaam.

“Ni kama mchakato wa uhakiki uko katika hatua za mwisho na kinachofanyika sasa ni kufanya majumuisho.
Siwezi kusema lini hasa tutamaliza, lakini kazi kubwa tumemaliza na kinachofanyika sasa ni majumuisho,” alisema Nchimbi.
Alisema utaratibu wa uhakiki huo wa vyeti ulianza rasmi Oktoba 10 na ulitarajiwa kukamilika Novemba 14, mwaka huu. Hata hivyo, alisema baada ya uhakiki huo wa vyeti, baraza hilo litawasilisha mrejesho wa matokeo ya uhakiki huo kwa taasisi husika zilizowasilisha vyeti vya watumishi wake kwa hatua zaidi dhidi ya watumishi watakaobainika kufanya udanganyifu.
“Sisi tunafanya uchambuzi wa vyeti hivi tulivyoletewa na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kuvihakiki, baada ya hapo tutatoa mrejesho kwa taasisi husika kuwa kati ya vyeti ilivyotuletea vingapi ni vya kughushi na taasisi hiyo ndio itakayochukua hatua,” alisema.
Hata hivyo, alifafanua kuwa kwa mujibu wa utaratibu wa Necta, mtu akifanya udanganyifu wa vyeti kwa kughushi au kutumia cheti kimoja kwa watu wawili, baraza hilo lina mamlaka ya kuwashtaki wahusika ikiwa ni pamoja na kumnyang’anya cheti mwenye cheti.
Alisema vyeti vyote vya kidato cha nne na cha sita vinavyotolewa kwa wahitimu ni mali ya Necta, hivyo endapo mtu akivitumia kinyume na inavyotakiwa baraza hilo lina mamlaka ya kumnyang’anya mhusika cheti hicho na kumshtaki.
Hivi karibuni, serikali ilitangaza rasmi kuanza kampeni ya kuwashughulikia na kuwaondoa katika utumishi wa umma watumishi wote walioajiriwa katika sekta hiyo wakitumia vyeti bandia.
Kutokana na kuanza kampeni hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano iliwataka watumishi hao waanze kujitathmini na kuanza kujiondoa wenyewe kabla ya kufikiwa na mabadiliko makubwa ya kusafisha sekta ya elimu na utumishi wa umma yanayokuja nchini.
Tayari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki ameiagiza Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu (Utumishi) kuwachukulia hatua stahiki watumishi watakaobainika kutumia vyeti visivyo vyao ili kupata ajira serikalini.
Naye Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu (Utumishi), Leonard Mchau alisema ni kosa la jinai kughushi vyeti kwa lengo la kujipatia kazi, hivyo endapo mtu atagundulika ameghushi vyeti atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi.
Hata hivyo, tayari kuna baadhi ya taasisi zimebainika kuwa na watumishi walioghushi vyeti ikiwemo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambayo ilihakiki watumishi 704 na kati yao 219 waligundulika kuwa waliajiriwa kwa vyeti vya kughushi.