Mchungaji wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo(Picha ya mtandao)

MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi, Anthony Lusekelo maarufu kama Mzee wa Upako, amesema licha ya kupatwa na mikasa mbalimbali, hajavunjwa moyo bado anaendelea na kwamba huu ni mwaka wa kucheka sawa sawa na lilivyo jina lake.
Alisema hayo ikiwa ni baada ya kuingia matatani na vyombo vya dola kutokana na kudaiwa kumfanyia vurugu jirani yake katika tukio lililotokea mwishoni mwa wiki na kuripotiwa na mitandao ya kijamii, huku picha zikimuonesha Mchungaji Lusekelo akirushiana maneno makali na jirani huyo aliyesikika sauti.

Alisema haiogopi jela, bali anaogopa kuvunja sheria za nchi na wala alipokamatwa na Polisi haikumtisha wala kumvunja moyo, kwani viongozi wa dini wamekula kiapo hadi kufa.
Lusekelo aliyasema hayo jana wakati akihubiri katika kanisa hilo lililoko Ubungo Kibangu, Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam, ambako alitumia takribani saa moja na kutoa mahubiri huku akisema hayumbishwi na matukio anafanya kazi ya injili.
Mara baada ya kuingia ibadani hapo, Mchungaji Lusekelo alianza kwa kipindi cha kusifu huku waumini waliofurika katika kanisa hilo wakimiminika kwenda mbele kutoa sadaka kisha kuanza mahubiri.
Aliwaambia asingependa kusema chochote kuhusu sakata lililomkuta, bali wakimaliza kusema yeye ndipo atakapoanza kusema na kwamba mwaka huu hawezi kuumaliza kwa huzuni, bali ni wa furaha kama jina lake lijulikanavyo kwa kabila la Kinyakyusa na wakati wote ana furaha.
“Sitaki kuzungumzia huko sana, ninafanya kazi ya Mungu, watu wanataka kuuza magazeti wanaandika taarifa zangu (Lusekelo), huku wakiandika vichwa vya habari eti Askofu matatani... matatani babu yao,” alisema Mzee wa Upako huku akisisitiza kuwa, “mbona yapo matukio makubwa zaidi katika kanisa lake na hayapewi kipaumbele kwa habari za mbele kama ilivyokuwa kwa tukio lililomkumba.”
Alihoji kuwa vyombo hivyo vya habari vimekosa taarifa mbalimbali za uchumi hata za biashara zilizopo nchini na kuamua kuandika kwa wingi na kwa uzito, akidai kwa kufanya hivyo kumeendelea kumpa umaarufu mzito.
Alisema unapowauliza waandishi kuhusu habari hizo nyingine, utawasikia kuwa habari sio mbwa kumng’ata binadamu maana ni jambo la kawaida, lakini binadamu anapong’ata mbwa hiyo kwao ndio taarifa.
Aidha, alisema wapo waliosema kuwa Mzee wa Upako alikuwa anatukana, alidai kuwa matusi yake yote ni maandiko na anayetaka ufafanuzi wowote akipata nafasi amuulize yameandikwa katika vitabu gani li apate kuelewa.
Alisema mpumbavu sio tusi hayo ni maelezo na Yesu alitukanwa sana, na hata ushenzi si tusi lina maana pana ya kwamba huna hofu ya Mungu, mjinga ana dhambi ya mauti, inayomsubiri kwenda peponi.
Hata hivyo, aliwausia waumini wa kanisa hilo kuwa kamwe wasimtukane mtu kwa umbo ama rangi yake kwa kuwa hakupenda kuzaliwa hivyo na waishi hivyo kwa kutenda mema kwa kuwa ufalme wa Mungu watauona.
Alisema tangu kutokea kwa tukio amekuwa akipigiwa simu na watu ambao hakuwategemea huku waandishi wakimtaka kuzungumzia chochote wakiwamo waandishi wa habari ambao alisema walikuwamo ndani ya kanisa hilo jana.
Akifafanua kilichotokea siku hiyo, alieleza kuwa alitoka saa 11 alifajiri bila kufafanua alikuwa akitokea wapi, ndipo alipokutana na watu wawili akiwemo Mmasai na dada mmoja alipowauliza wanatokea wapi katika eneo hilo ambalo wakazi wengi wa huko hutoka na magari yao, ndipo ugomvi ulipoanzia.
“Hawa watu wa magazeti wanataka kuuza magazeti, barabara hiyo nimeijenga mimi hivyo nilikuwa na haki ya kuwauliza maana ni kibarabara... washenzi wakubwa wanaandika tu, halafu wanasema nimewatukana majirani kule hakuna jirani hajui wanaingia saa ngapi na wanatoka saa ngapi na hakuna hata habari za asubuhi. Kila mmoja anatumia gari lake,” alieleza Mzee wa Upako.
“Hata vijana wa Sirro waliponikamata haijaniumiza, kunitisha wala kunivunja moyo kwani hata Yesu alikamatwa. Viongozi wa dini wamekula viapo hadi kifo, hawaogopi jela, anaogopa kuvunja sheria za nchi,” alisema.
Alisema cha kushangaza kasi ya waumini wake imeongezeka na jana walijitokeza kwa wingi. Walimpigia makofi mara kwa mara alipokuwa akizungumza.