Rais Magufuli na mgeni wake, Rais Edgar Lungu wa Zambia wakati mgeni huyo akiondoka nchini kurejea nyumbani kwake jana, kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.

RAIS wa Zambia, Edgar Lungu ameitahadharisha Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kuwa Wazambia hawabanwi na urafiki uliopo kati ya nchi hizi mbili kupitisha mizigo yao katika bandari ya Dar es Salaam, bali wanaendelea kufanya hivyo kutegemeana na ufanisi unaofanywa na mamlaka hiyo.

Akizungumza baada ya kutembelea baadhi ya vitengo vya bandari hiyo jana, Rais Lungu alisisitiza nchi yake itaendelea kupitisha mizigo kwenye bandari hiyo kama itaendelea kutoa huduma kwa ufanisi mkubwa kuliko bandari zingine zilizoko katika ukanda wa kusini mwa Afrika.
“Mimi na Rais Magufuli (John) tuna urafiki wa karibu, nchi mbili hizi pia zina urafiki wa muda mrefu, lakini Wazambia hawapitishi mizigo yao katika bandari hii kwa sababu ya urafiki wetu, bali wanachohitaji ni urahisi na uharaka wa kutoa na kusafirisha mizigo yao. “Pia hatuwaungi mkono kibiashara eti kwa sababu tu nchi mbili hizi tuna uhusiano mzuri, bali tunaangalia ni wapi ambako wanatoa huduma kwa haraka na kwa ufanisi...kwani naamini hata tusipowapa biashara undugu wetu wa damu utaendelea, lakini hatuendi kwingine tunakuja hapa kwa sababu ya ufanisi,” alisema Rais Lungu.
Rais huyo pia aliitahadharisha mamlaka hiyo kuwa wanatakiwa kuhakikisha kila siku wanabuni namna ya kuboresha huduma zao kwa kuwa kuna nchi jirani pia zinatoa huduma kama wanayotoa wao na ambao wangependa kupata biashara zaidi.
“Changamoto mliyo nayo ninyi watu ni kuhakikisha mnatoa biashara yenye kuhimili ushindani, huduma zetu ziwe za kisasa, maana kuanzia magharibi hadi mashariki kuna watu wanatoa huduma kama hizi. Hata sisi tungependa kutumia bandari ambayo ina ufanisi sio kwa kwa sababu ya urafiki wa kisiasa,” alisema Rais Lungu.
Alisema ndio maana mkutano wake alioufanya na Rais Magufuli walisisitiza ufanisi katika maeneo ambayo yanaunganisha nchi hizo kibiashara ili kuharakisha maendeleo kwa nchi hizo mbili.
Rais huyo pia alisema mambo hayo pia wameyazungumza juu ya Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (Tazara) na Bomba la Mafuta la Tanzania na Zambia (Tazama).
Alisema yeye hupenda kuona ubora na ufanisi katika biashara.
“Rais Magufuli mnamwita tingatinga kwa sababu hana utani na watu wanaoboronga, ni kama tunafanana naye maana hata mimi nasimamia maagizo yangu, hivyo nawatakeni mwongeze ufanisi kwa taasisi hii ili tuendelee kuwapa biashara,” alieleza.
Akielezea utendaji wa bandari hiyo juu ya huduma zinazofanywa na Zambia kupitia bandari hiyo, Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko alisema Zambia inasafirisha madini ya shaba na pia inaagiza mafuta yasiyosafishwa na yaliyosafishwa pamoja na mbolea kupitia bandari hiyo.
“Kwa miaka mingi Zambia imekuwa nchi ya kwanza kusafirisha tani nyingi kupitia bandari hii,” alisema Kakoko na kutoa mfano kuwa mwaka 2015 Zambia ilichangia mizigo inayopitishwa bandarini hapo kwa asilimia 36 ya tani milioni 5.2 za shehena zilizopitishwa bandarini hapo.
Alisema idadi ya mizigo inayosafirishwa na kuagizwa na Zambia imekuwa inaongezeka kila mwaka na akatoa mfano kuwa mwaka 2011 Zambia ilipitisha shehena ya tani 1,546,205 na mwaka 2015 ilipitisha shehena ya tani 1,903,979.
Kakoko aliipigia debe bandari yake kuwa huduma zake zinazidi kuboreka kila siku na sasa muda wa kupakua kontena umepungua kutoka siku 32 mwaka 2008 hadi kufikia siku 11 na muda wa meli kukaa bandarini ikipakua mzigo ni siku 2.4.
Uboreshaji mwingine ambao mkurugenzi huyo alimweleza Rais Lungu ni wa mfumo wa kufanya malipo sasa unafanyika kwa njia ya kielekroniki. Pia alisema ulinzi umeimarishwa zaidi na kamera 400 za CCTV zimefungwa maeneo mbalimbali ndani ya bandari hiyo.
“Vitendo vya wizi wa mizigo ndani ya bandari yetu imekuwa ni historia, havipo tena,” alisema Kakoso.