Amiri Jeshi Mkuu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, amefanya ziara ya kushtukiza katika Gereza la Ukonga jijini Dar -Es - Salaam na kupiga marufuku uuzwaji wa sare za majeshi nchini humo na watu binafsi na kutaka wale wote wanaouza sare hizo wazikabidhi kwa majeshi husika mara moja.

Rais Magufuli amepiga marufuku hiyo kufuatia maelezo kutoka kwa baadhi ya askari wa Jeshi la Magereza kuwa wamekuwa wakinunua sare za jeshi hilo kutoka kwa watu binafsi kinyume na taratibu za majeshi na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwachukulia hatua mara moja wale wote watakaobainika kuuza sare za majeshi.
Hali kadhalika Rais magufuli amepiga marufuku kwa majeshi yote nchini mwake kuingia ubia na watu binafsi kupangisha ama kuuza maeneo yao kwa ajili ya kufanya biashara na kutaka maeneo yote ya majeshi yabaki katika jeshi husika.''Haiwezekani sare za majeshi yetu hapa nchini kuuzwa na watu binafsi hilo haliwezekani kamwe labda baada ya kumaliza muda wangu , amesema Rais magufuli''
Aidha Rais Magufuli ametoa shilingi Bilioni Kumi kwa Jeshi la Magereza kwa ajili ya kujenga nyumba mpya zitakazotumika kwa ajili ya makazi ya askari wa Jeshi la Magereza katika Gereza la Ukonga jijini DSM.
Hatua hiyo inafuatia kilio cha askari Magereza kuwa wengi wao wamekuwa wakiishi uaraiani kitu ambacho ni tofauti na taratibu za majeshi na hata kuzorotesha utendaji kazi wa askari wa Jeshi hilo.
Amiri Jeshi Mkuu na Rais Dkt. John Pombe Magufuli pia ameagiza Jeshi la Magereza kuhakikisha wafungwa wanatumika katika uzalishaji mali badala ya mfumo wa sasa ambapo baadhi ya wafungwa wamekuwa wakitumia rasilimali za serikali bila kuzifanyia kazi.
Rais Magufuli amewahakikishia Maafisa na Askari wa Jeshi la Magereza kuwa serikali itaendelea kuboresha maslahi yao na vitendea kazi kama inavyofanya kwa majeshi mengine nchini Tanzania