Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, Jumamosi ijayo anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye uchangiaji damu salama katika viwanja vya Mwembeyanga, Temeke Dar es Salaam.
Mratibu wa shughuli hiyo, Suleiman Khamisi, amewaambia waandishi wa habari kwamba utaoaji huo wa damu ulioandaliwa na Taasisi ya Jumiiyatul Akhlaaqul Islaam (JAI)
inayojihusisha na kuhudumia wagonjwa hospitalini kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Temeke, utakuwa wa siku mbili, Jumamosi na Jumapili.
“Atakayefunga shughuli hii adhimu ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, Jumapili,” alisema Suleiman.
Alisema wanatarajia kwamba watu takribani 7,000 watashiriki katika utoaji damu ili kukusanya wastani wa uniti 3,000 za damu.
Suleiman alisema wameanza kupokea wageni kutoka sehemu mbalimbali za Tanzania ambao ni wanachama wa JAI zaidi ya 1,000 na ambao wamekuja kwenye mkutano wao wa ndani kabla ya kushiriki kwenye shughuli hiyo ya utoaji damu.