MKUU wa Mkoa Dar es Salaam, Paul Makonda amezindua nembo ya I love Dar (Naipenda Dar), inayobeba dhana nzima ya utalii wa ndani hususan mkoa wa Dar es Salaam.
Uzinduzi huo ulifanyika juzi usiku huku ukishuhudiwa na mamia ya watu, waliojitokeza kwenye eneo la baa ya Element iliyopo Oysterbay, Kinondoni.
Akizungumza baada ya kukata utepe kuashiria uzinduzi wa nembo hiyo, Makonda alisema ni hatua nzuri kwa wadau binafsi kujitokeza na kuendeleza mazuri kwa mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema nembo hiyo ya I love Dar, inahamasisha kuendeleza uzuri wa mkoa wa Dar es Salaam, ikiwa ni pamoja na kutangaza kila aina ya kivutio chake.
Alisema vipo vitu vya asili ambavyo vinatumiwa kama utalii, hasa kuanzia majengo ya kizamani hasa maeneo na mjini, makumbusho za taifa zenye kuhifadhi historia ya mkoa pamoja na mengineyo.
Alisema nembo hiyo inaenda mbali hadi kuhamasisha masuala ya kimaendeleo ya Dar es Salaam likiwamo suala la usafi.
"Najua I Love Dar ni nembo ambayo ina maana kubwa sana kwa wananchi kuipenda Dar ikiwa ni pamoja na kufanya mazuri kwa ajili ya mkoa huu kama vile kutangaza vivutio, kuzingatia usafi na mengine yote mazuri,” alisema Makonda.
Meneja wa Baa ya Element, Kenzie Mackezie alisema katika kuhakikisha kuwa inaunga mkono sera ya kuendeleza utalii wa ndani, imeamua kuanzia kwa kubuni nembo hiyo.
Alisema hata majiji makubwa duniani kama vile New York nchini Marekani, yana nembo ya I love New York na kwa hapa nchini kuandika I love Dar ni mwanzo wa kuliendeleza Jiji la Dar es Salaam kwa kuanzia kwenye utalii.