WADAU wa habari nchini wamemuomba Rais John Magufuli atoe agizo la kusogezwa mbele Muswada wa Sheria ya Huduma ya Habari wa mwaka 2016 hadi Februari mwakani kama ilivyoombwa na wanahabari kupitia Jukwaa la Wahariri (TEF) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii.

Aidha, imeelezwa pia kuwa Mwenyekiti wa kamati hiyo, Peter Serukamba ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni jipu na kwamba amevuruga mchakato wa muswada huo.
Katika maoni yao kwenye mkutano ulioandaliwa na TEF kwa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini jana Dar es Salaam kujadili muswada huo, wanahabari wameonesha masikitiko yao kwa Serukamba baada ya kudai kuwa muswada huo ni mzuri wakati wanahabari wenyewe hawajapata nafasi ya kuujadili na kuutolea maoni.
"Namuomba Rais, kwa hali ilivyo sasa afanye uchunguzi ni nani wazalendo wa kweli kati ya waandaaji wa muswada huo na wana habari... pia namuomba Rais atoe maagizo ya kusimamisha muswada huu," alisema Mwenyekiti mstaafu wa jukwaa hilo, Absalom Kibanda ambaye pia ni Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Magazeti ya New Habari.
Alidai Serukamba amekiuka misingi ya kazi yake ya kuisimamia serikali kama Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati, badala yake anasimama upande wa serikali, pia akidai kuwa watendaji wa serikalini wanamsukuma Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Nape Nnauye kutekeleza matakwa yao.
Jese Kwayu wa The Guardian Limited alisema anasikitishwa na msimamo wa Serukamba akidai amekuwa si mwenyekiti, bali kuizungumzia wizara husika.
"Kama kuna mtu ambaye anavuruga mchakato huu ni Serukamba, anataka usonge mbele tu... ana maslahi nje ya hayo," alisema Kwayu.
Katibu wa TEF, Neville Meena alisema muswada huo unahitaji mjadala wa kina kutoka kwa wanahabari wenyewe, kwani unakwenda kutengeneza msingi wa miaka kadhaa.
Mhariri Mtendaji wa Kampuni ya Jamhuri, Deodatus Balile alisema wanaomba nyongeza ya muda kwa sababu muda hautoshi kwani waliona muswada huo ukajadiliwe hadi mikoani ili kushirikisha wadau wote na kupata maoni yao kwani asilimia 70 ya waandishi wa habari wako mikoani.
"Leo kwa mfano tumekutana na wahariri, kwa hiyo tunaona tutakavyopata maoni mengi itasaidia kupata sheria bora, wadau wa habari wanaonekana na Kamati ya Serukamba kwamba tunavutavuta miguu, hapana sheria hii inagusa wadau wengi hivyo inahitaji muda zaidi," alisema Balile.