MKE wa Rais, Mama Janeth Magufuli aliyekuwa amelazwa katika wodi ya Sewahaji ya Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam, ameruhusiwa na kurejea nyumbani jana baada ya afya yake kuimarika.

Taarifa kwa vyombo vya harai iliyotolewa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, ilisema kabla ya kuondoka katika wodi ya Sewahaji alikokuwa amelazwa Mama Janeth aliwashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa matibabu mazuri aliyoyapata na aliwashukuru Watanzania kwa kumuombea afya njema.
“Namshukuru Mungu, afya yangu imeimarika, pia napenda kuwashukuru madaktari na wauguzi, nimepata huduma nzuri maana siku nilipoletwa hapa nilikuwa sina fahamu na hali yangu ilikuwa mbaya lakini mmenipigania na leo narudi nyumbani nikiwa na afya imara,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Mama Janeth aliongeza kusema, “Naomba pia niwashukuru Watanzania wote kwa kuniombea, nawahakikishia kuwa sasa nipo vizuri na madaktari wameniruhusu nirudi nyumbani ambako nitamalizia matibabu yangu.”
Taarifa hiyo iliendelea kusema Mama Janeth alilazwa hospitalini hapo tangu Novemba 9, mwaka huu baada ya kuugua ghafla na kupoteza fahamu.