RAIS John Magufuli ameongoza mamia ya waombolezaji mkoa wa Dar es Salaam, kuaga mwili wa Spika mstaafu wa Bunge, Samuel Sitta (73), wakiwamo marais wastaafu Benjamin Mkapa, Jakaya Kikwete na wake zao.
Sitta alifariki Jumatatu Novemba 7, akiwa katika matibabu nchini Ujerumani ambapo alikuwa akisumbuliwa na saratani ya tezi dume, mwili wake uliwasili nchini juzi. Wengine waliokuwapo katika hafla hiyo ya mazishi ni Makamu wa Rais wa Awamu ya Nne, Dk Mohamed Gharib Bilal na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Wengine ni mawaziri wakuu wastaafu Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi (NEC), Damian Lubuva, Katibu Mkuu Kiongozi John Kijazi na aliyekuwa Naibu Spika wakati Sitta akiwa Spika wa Bunge, Anne Makinda na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba.
Pia, mawaziri na viongozi wengine mbalimbali wa taasisi za serikali, vyama vya siasa na watu mashuhuri mbalimbali walitoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Sitta katika viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam jana.
Wachungaji wanena
Mwili wa Sitta uliwasili katika viwanja hivyo ukitokea nyumbani kwake Masaki jijini Dar es Salaam saa mbili asubuhi kwa msafara wa heshima ya kiserikali na kuanza kwa ibada iliyoongozwa na Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la KilutheriTanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Mchungaji Chediel Lwiza akisaidiwa na Mchungaji wa Kanisa hilo Kinondoni alipokuwa akiabudu Sitta, Mchungaji Ismail Mwipile.
Akihubiri katika ibada hiyo, Lwiza aliwataka watumishi wote wa dini, serikali na sekta binafsi kutumikia watu kwa uaminifu kwa kuhudumia bila kuangalia nini unapata kwa huduma unazotoa.
Wasifu wasomwa
Akisoma wasifu wa marehemu Sitta, Katibu Mkuu Utumishi, Dk Laurean Ndumbaro alisema alizaliwa Desemba 18, 1942 mkoani Tabora na mwaka 1950 mpaka 1953 alisoma shule ya msingi Urambo na mwaka 1954 alisoma shule ya msingi Sikonge.
Alisema mwaka 1958 mpaka 1963 alisoma shule ya sekondari ya wavulana ya Tabora na mwaka 1964 alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusomea shahada ya Sheria na kuhitimu mwaka 1971 na mwaka 1976 alijiunga na masomo ya Stashahada ya Utawala nchini Uswisi.
Ndumbaro alisema Sitta ameacha mjane ambaye ni mbunge wa jimbo la Urambo Mashariki, Margareth Sitta na watoto watano.
Aidha, katika utumishi wa serikali alianza mwaka 1967 na kushika nyadhifa mbalimbali ikiwemo Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji (TIC) mwaka 1996 mpaka 2005 aliposhika wadhifa wa Uspika wa Bunge la tisa la kasi na viwango.
Alisema katika kipindi hicho, Sitta amewahi kuwa mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro na Iringa na akiwa waziri wa ujenzi ndipo lilijengwa Daraja la Selander na Uwanja wa Ndege wa kimataifa Julius Nyerere (JNIA).
Mtumishi wa umma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Angella Kairuki akizungumza kwa niaba ya serikali alisema Sitta alifanya kazi katika utumishi wa umma kwa uzalendo kwa miaka 49 ya uhai wake na kuandika historia yake mwenyewe.
Alisema Sitta anaingia katika kumbukumbu za taifa kutokana na kuimarisha mhimili wa Bunge alipokuwa Spika wa Bunge bila kujali itikadi za vyama pamoja na mchango wake alipokuwa mwenyekiti wa bunge la katiba mwaka 2014.
Kairuki alisema Sitta pia anajulikana katika nchi za Afrika Mashariki kwani alishiriki katika harakati za nchi hizo kuingia katika soko la pamoja na majadiliano ya matumizi ya sarafu moja kwa nchi hizo.
Sitta kama wakili
Jaji Kiongozi Ferdinand Wambali, alitoa salamu za Mahakama kwa niaba ya Jaji Mkuu kutokana na Sitta kuwa mwanasheria na kutokana na unyenyekevu wake ndio maana wanathamini mchango wake miaka 21 iliyopita akiwa waziri wa sheria aliitwa kutoa ushahidi wa kesi ya ajali ya barabarani aliyoshuhudia.
Alisema wakati kesi zinaanza kusikilizwa saa tatu asubuhi, Sitta alifika saa moja asubuhi ili kutoa ushahidi kutokana na kushuhudia ajali huku akiwa karibu na idara hiyo kwa kutoa maoni yake kwa maandishi au kufika kwa uongozi wa Mahakama ili kuboresha utoaji haki.
“Alikuwa akiendesha ofisi yake ya uwakili na kuongoza watumishi wake katika maadili kwa kufuata kanuni na taratibu za kazi zilizofanya kuteuliwa kwa majaji wawili kutoka katika ofisi yake,” alisema.
Msaada kwa watu
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alipotoa salamu za wakazi wa mkoa huo, alisema alimfahamu Sitta mwaka 2008 kupitia kwa Waziri wa Sheria na Katiba wa sasa, Dk Harrison Mwakyembe na mwaka 2010 alipokosa ada ya kusoma Chuo cha Ushirika Moshi alifika katika ofisi za Chama Cha Mapinduzi kuomba msaada.
Alisema alipokutana na Sitta alimsomesha mpaka alipomaliza masomo yake yote na kumfanya mtoto wa familia yake kwa kuwatambulisha kwa wanawe na mpaka kumsimamia shughuli zote alipokuwa anaoa, hivyo yeye anamuona ni baba yake.
“Alipokuwa akiondoka, niliomba naye na kumpakiza katika gari la kubeba wagonjwa nikijua atarejea nchini salama, lakini alifariki hivyo naomba ili kuwaenzi watu kama hawa katika makao makuu ya nchi Dodoma kuwe na makaburi kwa ajili yao kama ilivyo katika nchi nyingine zenye makaburi ya viongozi ambapo watu wanafika na kujua historia zao, alisema.
Shukurani ya familia
Akitoa shukrani kwa niaba ya familia, mtoto wa marehemu Caroline Sitta alishukuru wote walioshiriki kwa namna moja au nyingine kiroho na kupata matibabu kwa baba yao, ikiwemo serikali na ofisi ya bunge pamoja na viongozi wa kiroho.
Alisema kubwa la kujifunza kwa baba yao na alisisitiza wakati wote ni kuwa wakweli na kusimamia kile wanachokiamini na aliwaeleza hata wakiwa katika matatizo kuvaa ngozi ngumu na kusimamia neno la Mungu ambalo ni Ayubu 19:25 ambalo baba yao alikuwa akilisoma wakati wote.
Sifa zake kuu
Viongozi wa Serikali na wa Bunge wamemuelezea Spika mstaafu wa Bunge la Tisa (2005-2010), Samuel John Sitta (75) kuwa ni mtu asiyekuwa mbinafsi, mlezi na kiongozi aliyesimamia alichokiamini kwa viwango, kasi na demokrasia ya kweli.
Viongozi hao wakizungumza kwa nyakati tofauti wakati wakitoa salamu za rambirambi bungeni jana kwenye kikao maalumu cha Bunge cha kutoa heshima za mwisho kwa Sitta, walisema wakati wote alijali watu, hakuwa na uchu wa mali, aliliunganisha Bunge bila kujali itikadi za kidini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa salamu za rambirambi, alisema Sitta ambaye amelitumikia Taifa kwa nyadhifa mbalimbali ikwiemo Ubunge wa Urambo kwa miaka 20, alikuwa ni kiongozi aliyetukuka.
“Alitukuka katika utumishi wake, tulivyopokea taarifa Serikali tulishtuka sana. Sitta alisimamia ukweli, demokrasia na elimu aliyoipata aliitumia kwa manufaa ya wote,” alisema Majaliwa.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Job Ndugai alimzungumzia Sitta kama kiongozi mwenye uthubutu na aliposimamia jambo aliweza kukwepa vigingi na vizingiti.
Ndugai alisema alitengeneza timu ya Wabunge ya Kuhuisha Kanuni za Bunge mwaka 2006, yeye (Ndugai) akiwa mwenyekiti wa kamati hiyo na ndio mapokeo ya kanuni zinazotumika katika vikao vya Bunge sasa.
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema) alisema kambi hiyo nje na ndani ya Bunge walimjua Sitta kama kiongozi asiye na ubaguzi wa kiitikadi.
Alisema aliamini katika mabadiliko ya Bunge kwenda kwenye ubora zaidi na aliwajaza aliowaongoza matumaini na aliunganisha makundi yote.
“Kuna wakati tulikuwa na wakati mgumu kujua kama bado ni kada wa CCM au la. Tukizungumza naye tunapata matumaini, baadaye tunatambua kuwa, bado ni kada wa CCM,” alisema Mbowe na kushangiliwa na wabunge wote.
Alisema Sitta aliwaongoza na kuwapigania watu wote na pia kwa nafasi yake, alitaka Bunge lisimame kama mhimili wa kuidhibiti Serikali na alitetea Serikali alipostahili. Mbowe alisema funzo kubwa kwa msiba huo ni kwa waliobaki kujitafakari baada ya safari kama ya Sitta, watu watakuzungumzaje.
“Sitta tunamzungumza kwa dhati ya moyo wetu. Alituunganisha wote, kazi aliyotuachia tumalize. Ameacha Katiba, wananchi wanataka Katiba itakayowaunganisha Watanzania,” alisema. Mbowe alisema vyeo ni dhamana, “Tunapita, tupendane wakati wote. Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya Sitta. (akamgeukia mke wa Sitta) Margareth wewe ni mama mpole, mnyenyekevu ni tunu aliyokupa Mungu, hukuniona mtoto, bali kiongozi, nakumbuka ulikuja ofisini kwangu ukataka nikusaidie tuwaunganishe wabunge wanawake, mama pole”.
Katibu wa Wabunge wa CCM, Jason Rweikiza, alisema Sitta hakupenda majungu, kujinufaisha bali alipigania wanyonge, aliwafundisha kufanyakazi kwa kasi na viwango.“Hakika Sitta ni kisima cha hekima,” alisema Rwekiza akikiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu(Chadema) alisema Sitta ni mmoja wa miamba ya Bunge na ilikuwa haki na sawasawa kumuaga katika ukumbi wa Bunge ambao yeye (Sitta) akiwa Spika wa Bunge la Tisa na Mwenyekiti wa Bunge la Katiba, aliutawala vizuri.
“Alilitoa Bunge kutoka katika kivuli cha Serikali. Alitaka Bunge lenye meno, linaloisimamia Serikali na kuidhibiti Serikali kama mhimili wa dola na si msindikizaji wa mihimili mingine. Hakuwa kibaraka wa mtu yeyote tangu kijana alionesha mtu mwenye msimamo huru, tumuenzi kwa kujiuliza, hili ni Bunge alilolitaka Sitta,” alisema Lissu.
Naye mwakilishi wa Chama cha Wananchi (CUF), Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Mngwali, alisema hakuwahi kufanya kazi kwa karibu na Sitta, lakini wafanyakazi na wabunge aliozungumza nao walisema Sitta alisikiliza shida za wadogo mpaka wakubwa na alikuwa kiongozi wa wanyonge.
Mwakilishi wa ACT-Wazalendo, Kabwe Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini, alitoa salamu kwa namna ya utenzi, akimzungumzia Sitta, ambaye mwili wake ulikuwa umelala ndani ya jeneza mbele ya kiti cha Spika.
Zitto alimuelezea Sitta kama shujaa wa wote wanaoamini uwajibikaji wa kitaasisi, mwanamageuzi wa kweli na Spika wa moyo wa Watanzania.
“Unaweka rekodi hata ulipolala katika jeneza lako, “The People’s Speaker (Spika wa Watu). Ulikuwa baba, mlezi, mume mwema, ulikuwa babu, hata uliokwaza nao wanajua hilo,” alisema Zitto.
Alisema Sitta alipopokea Uspika, aliboresha mengi na kurejesha Bunge katika hadhi yake kwa mujibu wa Katiba.
“Mwaka 2009 nikiwa na miaka 29 tu, tulikwenda kuonana na Rais, tukaongozana nawe, babu uliniambia, mimi sasa ni alasiri, nyie ndio saa sita. Bado tunaisikia sauti yako katika kiti cha Spika, ukiwataka mawaziri wajibu maswali kwa ufasaha.Wewe ni kielelezo cha demokrasia ya vyama vingi bungeni, katika uongozi wako, walio wengi walishinda, lakini wachache walisikilizwa,” alisema Zitto kwa majonzi.
Kuhusu msamaha, alisema upo wakati Sitta alimkosea Cheyo (John) kwa kumtoa kimakosa Bungeni lakini baada ya kugundua alikosea, alimuomba radhi na kusema alighafilika kwa kuwa na msongo wa mawazo maana kuna watu walikuwa wakipitapita jimboni kwake.
Mapambio yaliza
Baada ya mwili kufika mbele ya Kiti cha Spika na viti vya makatibu, huku kukiwa na utulivu, Wimbo wa Taifa ulipigwa na kufuatiwa na dua zilizotolewa na wabunge wenyewe kwa imani tofauti.
Dua kwa imani ya Kiislamu ilitolewa na Mbunge wa Magogoni, Pemba, Dk Yusuf Ali Suleiman (CUF), aliyetaka watu kuishi kwa amani na kumtegemea Mungu, kuondoa kiburi na chuki.
Dua kwa niaba ya Wakatoliki, ilitolewa na Mbunge wa Viti Maalum, Shally Raymond (CCM) na kwa niaba ya waumini wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) alitoa dua hiyo Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe.
Pamoja na kwamba dua zote ziligusa waombolezaji kwa namna tofauti, lakini dua ya Dk Mwakyembe, ambaye ni Waziri wa Katiba na Sheria, iliwaliza waombolezaji wengi, wakiwemo waandishi wa habari.
Dk Mwakyembe alianza kwa utulivu na sauti iliyobeba huzuni na alivyokuwa akiendelea kusali, sauti yenye kuashiria analia ilisikika na kubadilisha hali ya hewa ya ukumbi mzima.
Machozi yalishindwa kuzuilika machoni mwa wabunge, ndugu na watu wengine waliohudhuria tukio hilo la kumuaga Spika wa Tano wa bunge la Jamhuri ya Muungano jana, bungeni.
Dua ya Dk Mwakyembe iliwaliza watu wengi na wengine walishindwa kujizuia wakalia kwa sauti na kufanya ukumbi mzima wa bunge kutawaliwa na simanzi na giza nene huku jeneza la mwili wa Sitta likiwa mbele na kufikirisha kama vile huenda angesimama na kuona kinachoendelea.
Maandalizi Urambo
Vilio, simanzi na huzuni vilitawala jana nyumbani ambapo maandalizi ya msiba wa aliyekuwa Spika mstaafu wa bunge marehemu Samuel Sitta yanaendelea.
Akizungumza na gazeti hili msemaji wa familia, Peter Sitta alisema wananchi wamejiandaa kuupokea mwili chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa wa Tabora Tabora Aggrey Mwanri.
Alisema kuwa hadi sasa wakuu wote wa wilaya wa mkoa huo wamefika kuungana na familia kwa ajili ya maandalizi ya kuaga mwili na maziko.
Walioshiriki kuandika ni Theopista Nsanzugwanko, Dar; Gloria Tesha, Dodoma na Lucas Raphael, Urambo.