Wagombea urais wawili wakuu wa urais Marekani Hillary Clinton na Donald Trump wanakaribiana sana katika matokeo ya uchaguzi wa urais katika majimbo muhimu yanayoshindaniwa.
Ni vigumu kubaini nani atashinda Florida, na North Carolina.
Clinton ameshinda Virginia naye Trump akashinda Ohio.
Lakini mgombea wa Republican Bw Trump ameshinda majimbo mengi ya kusini mwa Marekani naye Bi Clinton akashinda majimbo ya kaskazini mashariki mwa nchi hiyo, kwa mujibu wa makadirio ya shirika la utangazaji la ABC News.
Chama cha Republican kinaonekana kuwa njiani kuhifadhi wingi wa wabunge katika Bunge la Wawakilishi.
Kama ilivyotarajiwa, Bw Trump ameshinda katika ngome za Republican katika majimbo ya Alabama, Kentucky, South Carolina, Nebraska, Indiana, West Virginia, Mississippi, Tennessee, Oklahoma na Texas, ABC News wanakadiria.
Bw Trump pia anakadiriwa kushinda Arkansas, Kansas, North Dakota, South Dakota, Montana na Wyoming.
Shirika hilo linakadiria Bi Clinton atashinda ngome za Democratic majimbo ya New York, New Jersey, Connecticut, Massachusetts, Maryland, Vermont, Delaware, Illinois, Rhode Island na District of Columbia.
Mshindi anahitaji kupata kura 270 kati ya jumla ya kura 538 za wajumbe ndipo atangazwe mshindi.

Voters cast their votes during the US presidential election in Elyria, Ohio, on 8 November.Image copyrightREUTERS

Upigaji kura umemalizika katika majimbo 39 na matokeo kamili yanatarajiwa mwendo wa saa 23:00 EST (04:00 GMT Jumatano - Saa moja asubuhi Afrika Mashariki), upigaji kura utakaomalizika Pwani ya Magharibi.

Matukio mengine makuu:

  • Bodi ya Uchaguzi Carolina Kaskazini imekubali kuongeza muda wa kupiga kura maeneo manane wilaya ya Durham ambapo kuna milolongo mirefu ya wapiga kura.
  • Mgombea wa Republican aliyeshindwa kwenye mchujo Marco Rubio amehifadhi kiti chake cha useneta Florida
  • Thamani ya pesa za Mexico, peso, imeshuka sana baada ya Trump kuonekana akiongoza Florida
  • Mtu mmoja alifariki kwenye ufyatulianaji wa risasi karibu na kituo cha kupigia kura jimbo la Azusa, California. Watu watatu walijeruhiwa.
Bw Trump, tajiri kutoka Manhattan, na Bi Clinton, anayetaka kuwa rais wa kwanza mwanamke Marekani, walipiga kura mapema Jumanne katika jiji la New York.
Bw Trump alizomewa alipofika kupiga kura yake Manhattan, akiandamana na mkewe, Melania, na bintiye, Ivanka.
Wawili hao wamekuwa wakifuatilia matokeo kutoka jiji la New York.
Bi Clinton atahutubia wafuasi Javits Centre, Manhattan naye Bw Trump atahutubu katika hoteli ya Hilton Midtown.
Maafisa wa polisi zaidi ya 5,000 wametumwa jijini New York kuimarisha usalama.
Utafiti wa maoni wa baada ya upigaji kura, uliofanywa na ABC News, unaonyesha wapiga kura 61% hawampendi Bw Trump nao 54% ndio hawampendi Bi Clinton.
Mapema Jumanne, Bw Trump kwa mara nyingine alikataa kusema iwapo atakubali matokeo.
"Tutaangalia tuone vile mambo yatakuwa," aliambia Fox News, huku akidai kwamba kumekuwa na kasoro hapa na pale kwenye uchaguzi.
"Ninataka kila kitu kiwe wazi."
Katika baadhi ya vituo, mitambo ya kupigia kura ilifeli na kwingine kukawa na milolongo mirefu, lakini yalionekana kuwa matatizo ya kawaida.
Bw Trump, aliyezua utata kuhusu kuaminika kwa shughuli ya uchaguzi kwa kudai kura "zitaibwa" mapema, pia amewasilisha kesi ya dharura Nevada.
Maafisa wa Republican wamemshtaki msajili wa wapiga kura wilaya ya Clark, wakidai jimbo hilo lilifungua vituo vya kupigia kura muda mrefu kuliko inavyofaa.
Lakini jaji ameitupilia mbali kesi hiyo.
Kando na kura za urais, Wamarekani wamekuwa pia wakipiga kura za Maseneta, wabunge wa Bunge la Wawakilishi na Magavana.
Viti vyote 435 Bunge la Wawakilishi vilikuwa vinashindaniwa, na ABC News wanakadiria kwamba bunge hilo litabaki chini ya udhibiti wa Republican.
Lakini theluthi moja ya viti Seneti, ambao Republican wamekuwa wanaongoza, pia vinashindaniwa, na Democratic wanatumai wanaweza kudhibiti bunge hilo.
Jumla ya Wamarekani 45 milioni, idadi kubwa zaidi kuliko awali, walijitokeza kupiga kura mapema.
Bw Trump na Bi Clinton wanapigania kumrithi Barack Obama wa Democratic.
Rais Obama haruhusiwi kuwania kikatiba baada ya kuhudumu mihula miwili ya miaka minne.
Rais mpya ataapishwa tarehe 20 Januari 2017.