MBUNGE wa Kiembe Samaki, Ibrahim Hassanali Raza (CCM) amewalaumu madereva wa mabasi yanayokwenda kwa haraka jijini Dar es Salaam kwamba hawazingatii sheria za barabarani.
Aidha, ametaka kujua muda kamili wa mabasi hayo kuanza kazi na kumaliza kazi kwa kuwa kumekuwa na usumbufu kwa wasafiri wanaotumia usafiri huo.

Raza alitaka kufahamu serikali itawachukulia hatua gani madereva hao na kueleza ni muda gani mabasi yanatakiwa kuanza kazi.
Akijibu swali hilo la msingi bungeni mjini hapa, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo alisema madereva wanaosimamiwa na Kampuni ya Uendeshaji wa mabasi hayo (Udart), wanapaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani kama kwa madereva wengine.
Jafo alisema tangu mabasi yaanze kutoa huduma, madereva 20 wamepewa onyo kwa makosa ya usalama barabarani na wawili wamefukuzwa kazi na wengine 40 wamekatwa mishahara kwa makosa mbalimbali yakiwemo ya usalama barabarani.
Alisema ili kudhibiti mwendo wa mabasi, vimefungwa vifaa maalumu katika magari ili kutoa ishara kwa dereva anapozidisha mwendo ambao ni kilomita 50 kwa saa. Kuhusu muda wa kuanza kazi, Jafo alisema mkataba baina ya Dart na mtoa huduma Udart umeainisha kuwa, mabasi hayo yanaanza kazi saa 11 alfajiri hadi saa sita usiku.