Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Siasa na Utawala, Dk Benson Bana
WASOMI wamewataka viongozi na wananchi katika nchi za Afrika ikiwamo Tanzania kutafsiri kauli zilizokuwa zikitolewa na Rais mteule wa Marekani Donald Trump wakati wa kampeni.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Siasa na Utawala, Dk Benson Bana alisema kauli za Trump kuhusu Afrika, waafrika na viongozi wa kiafrika zilikuwa na dalili za ukweli na kuwa sasa ni vyema kutafsiri kauli hizo ili kupia hatua za maendeleo na kutoingia matatani.

“Kauli zile zilikuwa ni maoni yake, lakini zilikuwa na dalili za ukweli, kwani pamoja na rasilimali zilizopo Afrika wanategemea misaada, kuna viongozi wanaong’ang’ania madaraka na mafisadi wanaoficha fedha nje ya nchi. “Hivyo kauli zake zichangize katika kuleta mabadiliko, tukemee ufisadi, rushwa, watu kutawala bila kuzingatia katiba na kukemea ugaidi na uhamiaji halamu,” alisema Dk Bana alipongeza hatua ya Rais John Magufuli aliyoichukua mara tu baada ya kuingia madarakani ya kutaka Tanzania kuacha kutegemea misaada na badala yake kujikita katika kukusanya mapato ambayo yataumika katika kutekeleza miradi ya maendeleo.
Naye Mshauri Mkuu wa chama cha ACT-Wazalendo, Profesa Kitila Mkumbo alisema kauli zilizokuwa zikitolewa na Trump kabla ya kuingia madarakani ni mambo ambayo yamekuwa yakipigiwa kelele na kukemea.
“Suala la viongozi kwenda kuficha fedha nje ya nchi, ni jambo ambalo hata sisi tulikuwa tunalipigia kelele na sio jambo jema kabisa, na mambo mengi aliyokuwa yakisemwa chini chini, Trump alipata ujasiri wa kuzungumza hadharani,” alisema.
Mkumbo alisema anaamini baadhi ya mambo ambayo Trump alikuwa akiyasema hayataweza kutekelezwa kutokana rais wa Marekani kutokuwa na mamlaka kubwa ya kuyatekeleza yale ambayo angetamani kuyatekeleza.
Alisema suala la wahamiaji ni jambo ambalo anaweza kulitekeleza na kutoa tahadhari kuwa kipindi cha uongozi wa Trump kitakuwa kigumu kuingia Marekani ukilinganisha na wakati wa uongozi wa Barack Obama.
“Ni lazima waafrika wakiwemo Watanzania ambao wanaishi nchini Marekani bila kuwa na vibali halali, wakajifunza kuanza na kutengeneza mazingira ya kuishi kwa kuzingatia sheria na taratibu, maana watakuwa na wakati mgumu na itakuwa ni vigumu kuingia Marekani,” alisema.
Trump ameibuka mshindi wa Uchaguzi Mkuu wa nchi hiyo, hivyo kuwa Rais wa 45 wa taifa hilo kubwa lenye nguvu kubwa ya kiuchumi na kijeshi na kumbwaga mpinzani wake wa Democrat, Hillary Clinton baada ya kupata kura 276 dhidi ya kura 218.