Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju
SERIKALI imewasilisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Namba 3 wa Mwaka 2016 ukiwa na marekebisho mapya, yakiwemo kuliondoa Bunge, Mahakama na majeshi yote na Usalama wa Taifa katika arodha ya watumishi wa umma, ambao mishahara, posho na marupurupu mengine, yataidhinishwa na Katibu Mkuu Utumishi.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), George Masaju alitoa kauli ya mabadiliko hayo jana bungeni wakati akiwasilisha muswada huo unaozifanyia marekebisho sheria tisa.
Kwa mujibu wa Marekebisho ya Sheria ya Utumishi wa Umma Sura ya 298, mamlaka, mihimili na taasisi zote za umma, kulipendekezwa kuongezwa kifungu cha 9A cha sheria kinachoweka masharti ya kuziondolea mamlaka ya kuidhinisha mishahara na marupurupu kwa watumishi na badala yake, kibali kingetolewa na Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma.
Masaju akifafanua kuhusu masharti ya watumishi wengine wa umma katika mishahara, posho na marupurupu, alisema Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais (Utumishi), atahusika na taasisi nyingine kwa uwiano sawa kama yalivyo mapendekezo ya muswada huo.
Alisema lengo kuweka usawa wa maslahi kwa watumishi wa umma kulingana na kazi wanazofanya kwa mujibu wa Kifungu cha 31(2) cha Sheria hiyo ya Utumishi wa Umma.
“Muswada huu unapendekeza kurekebisha kifungu hicho ili kuweka masharti yatakayowezesha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (Utumishi ) kuwa mamlaka ya kurekebisha na kuwianisha mishahara, posho na marupurupu mengine ya watumishi wote wa umma,” alifafanua Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Alisema mapendekezo mapya kwa kuzingatia maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, serikali imeyaondoa masharti hayo ya mishahara, marupurupu na maslahi mengine kwa Bunge, Mahakama, Jeshi la Ulinzi la Wananchi (JWTZ), Polisi, Magereza, Uhamiaji, Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Zimamoto na Uokoaji na Idara ya Usalama wa Taifa.
Kuhusu mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu, marekebisho yameelekezwa katika faini ambako sasa mwajiri atakayeshindwa kuifahamisha Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HELSB) kuwa mwajiriwa ni mnufaika wa mikopo ndani ya siku 28 baada ya kumwajiri mtumishi mwenye shahada au stashahada, atakuwa ametenda kosa la jinai. Maboresho hayo mapya yameeleza kuwa sasa adhabu yake itakuwa Sh milioni moja bila kifungo.
Muswada wa awali mapendekezo yalikuwa ni Sh milioni tatu na kifungo hicho cha miezi sita. Kuhusu makato kwa mkopaji, imependekezwa mnufaika aliyejiajiri alipe marejesho ya Sh 120,000 kwa mwezi au asilimia 10 ya mapato yake kutoka Sh 120,000 au asilimia 15 ya mapato yake. Hata hivyo, kwa mtumishi aliyeajiriwa hakuna marekebisho, mwajiri atakata asilimia 15 ya mshahara wa mhusika.
Masaju alisema pia serikali imezingatia maoni ya Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria kwa kufanyia marekebisho katika muda wa kuanza kulipa mkopo kwa wanufaika uwe mwaka mmoja baada ya kuajiriwa. Awali ilikuwa mara baada ya kuajiriwa. Kamati hiyo ilipendekeza mnufaika wa mkopo aliyejiajiri alipe Sh 100,000.
Alisema muswada huo umependekeza kuondoa mapendekezo kuhusu Mahakama kutoa amri ya kutaifisha gari linalojihusisha na kosa linalojirudia kwa mara ya pili na kuendelea hivyo hakutakuwa na kutaifishwa kwa gari. Ni marekebisho ya Ibara ya 35 ya Sheria ya Leseni za Usafirishaji.
Hata hivyo, mapendekezo ya kuongeza adhabu katika kosa la kutumia gari kinyume na leseni inayotolewa na chini ya Ibara hiyo imependekezwa faini iwe Sh 200,000 kwa mkosaji wa mara ya kwanza badala ya Sh 50,000, mara ya pili faini isiyopungua Sh 500,000 inayotajwa kwenye sheria ya sasa.
Kwa upande wa kosa la kughushi, leseni inapendekezwa adhabu iwe Sh 500,000 au kifungo gerezani kisichopungua miaka miwili. Faini ya sheria ya sasa ni faini isiyozidi Sh 50,000 au kifungo cha miaka mitano.
“Muswada unapendekeza adhabu ya mtu anayetenda kosa la kutoa taarifa za uongo ili kupata leseni itakuwa faini isiyopungua Sh 200,000 au kifungo gerezani kisichopungua miaka miwili badala ya faini isiyozidi Sh 50,000 au kifungo kisichozidi miaka mitano cha sasa,” alisema.
Katika Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), inapendekeza kuongezwa kifungu cha 40A kuweka masharti ya ufifishaji wa makosa ili mtu akitenda kosa kabla ya mahakamani, Sumatra imtoze faini isiyozidi nusu ya faini ya mahakamani.