Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Nov 9, 2016

Bunge laifunga mikono serikali

BUNGE limeukataa rasmi Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Ulaya (EU) na ya Afrika Mashariki (EPA) na kuishauri serikali isiusaini.
Limesema kama kutakuwa na nafasi ya majadiliano, basi marekebisho makubwa yafanyike kwa maslahi ya Taifa ili kwenda sambamba na sera ya kodi na ya uchumi wa viwanda ya nchi.

Aidha, wameishauri serikali kupeleka bungeni mikataba mingine inayogusa maslahi ya Taifa, ikiwemo ya gesi, mafuta na madini ili ijadiliwe na Bunge liishauri serikali kama ilivyofanya kwa mkataba huo wa EPA ili kuisaidia nchi isiingie katika mikataba ya kinyonyaji.
Mazimio ya Bunge yalifikiwa jana, bungeni mjini hapa baada ya wabunge kuujadili mkataba huo na kisha Spika wa Bunge, Job Ndugai kuwahoji wanaoafiki usainiwe na wasioafiki. Kwa mara ya kwanza na kwa kauli moja, wabunge wa upinzani walieleza misimamo yao na vyama vyao kuwa Serikali isiusaini mkataba huo kwa kuwa hauko kwa maslahi ya nchi.
Msimamo huo ulitawala mjadala kwa pande zote ikiwemo kwa wabunge wa chama Tawala (CCM) waliochangia pamoja na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, iliyowasilisha mkataba huo bungeni juzi na ulitakiwa kujadiliwa kesho, Alhamisi lakini umejadiliwa jana kutokana na juzi Bunge kuahirishwa kufuatia msiba wa Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa, Samuel Sitta.
“Kwa kauli moja Bunge linaishauri Serikali isisaini mkataba huu. Katika Mkutano wa Nne wa Bunge jambo hili lilikuwepo na ilionekana wabunge wapate nafasi ya kuishauri Serikali. Utakuwa na utaahira fulani mkataba huu ukasainiwa kwa jinsi ulivyo. Lo! Hapana haiwezekani,” alisema Ndugai akitoa maazimio ya Bunge baada ya kuwahoji wabunge.
Awali, katika mjadala kuhusu mkataba huo, Mbunge wa Mchinga, Hamidu Bobali (CUF) alisema chama chake cha Wananchi CUF kimewaagiza wabunge wake kuishauri serikali isiusaini mkataba huo.
“CUF imetuagiza kwamba huu mkataba tuukatae. Chama chetu kimefanya uchambuzi wa kutosha, imeona tujipange kwanza kabla ya kuusaini. Mikataba kama hii ya gesi na madini iletwe bungeni maana inagusa maslahi ya Taifa letu,” alisema Bobali.
Bobali alitaka taifa lijiulize kama bidhaa zetu zina viwango vinavyokidhi soko la Ulaya ama bidhaa za Ulaya ndizo zitatawala soko la Tanzania. Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM) alishauri mkataba huo usisainiwe kwa kuwa hautoi nafasi ya kwa nchi husika kuingia makubaliano ya kibiashara na nchi nyingine nje ya EU.
Hata hivyo, Lugora alishauri Serikali kutumia wataalamu wake kuchambua maeneo yenye shida katika mkataba huo yaboreshwe kama kutakuwa na nafasi hiyo.
“Kuna maeneo mazuri ila mambo makubwa ni mabaya, wabunge wa EALA (Bunge la nchi za EAC) nao wasikubali nchi zao zisaini kwani kuna maeneo unalenga kutuletea mambo ya ushoga, tusipokuwa macho sehemu nyeti za wanaume zitaingiliwa mheshimiwa Spika, tusikubali,” alisema Lugora na kushangiliwa na wabunge wengi. Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF) alisema mkataba huo ni msiba kwa Taifa na hauna faida kuujadili.
“Nimesimama hapa kama mzalendo wa Tanzania, mkataba huu umelenga kuingilia uhuru wetu na ni janga ambalo halivumiliki,” alisema Haji.
Mbunge wa Ubungo, Saeed Kubenea (Chadema), alisema mkataba huo ulipitia katika mamlaka kadhaa ikiwemo kikao cha makatibu wakuu, Baraza la Mawaziri kabla ya kwenda EALA na kushauri kabla Bunge halijaishauri Serikali isiusaini, upande mwingine wa uzuri wa mkataba huo ielezwe. Alishauri Serikali ifanye tena majadiliano upya.
Naye Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM) alisema mkataba huo hauna manufaa yoyote kwa taifa.
Alisema katika ukanda mwingine, zipo baadhi ya nchi hazijausaini ikiwemo Angola (Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika-SADC) na Nigeria na Gambia (Jumuiya ya Ushirikiano wa Uchumi Afrika Magharibi- ECOWAS).
Kwa upande wake, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), alishauri hatua ya mikataba hiyo kuletwa bungeni iendelee na kuhusu mkataba huo, alisema hautambui nchi kama nchi bali ukanda (jumuiya).
Alishauri kama EU ina nia njema na Tanzania, kupelekwe marekebisho kufafanua baadhi ya vifungu na kuruhusu nchi iingie EPA kwa matakwa yake na si vinginevyo.
“Mkataba huu ulivyo, unatugeuza sisi kuwa wazalishaji wao wa malighafi na kugeuka masoko kwao,” alisema Bashe na alikitaja kifungu cha 143 kuhusika na kuruhusu hilo na nchi itageuka soko la bidhaa za Ulaya bila faida kwa nchi husika.
Alisema, “Wao wana teknolojia na mitaji, sisi tuna malighafi, waje waanzishe viwanda hapa, tusigeuke wazalishaji wa malighafi na wanataka kuigawa Afrika maana makubaliano kwa Afrika Magharibi, hayafanani na Afrika Mashariki. Nampongeza Rais John Magufuli kwa kutokusaini mkataba huu”.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT Wazalendo) alisema Kenya wamesaini mkataba huo kwa sababu ya biashara ya maua na kutaka suala la kitaifa kama hilo wabunge wawe kitu kimoja na waitizame nchi.
Alishauri kwa namna ulivyo, serikali isiusaini. Zitto alisema ikiwa mkataba huo utasainiwa na bidhaa za EU zikaingia bila kodi, nchi itapoteza Dola za Marekani milioni 853 (Sh trilioni 1.8) kwa miaka 25 na nchi za EAC zitapoteza Sh trilioni nane.
Jumapili iliyopita, wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) waliwapa semina wabunge kuhusu mkataba huo na kuwashauri kuwa kwa namna ulivyo, haufai. Hata hivyo Kenya na Rwanda zimekiuka makubaliano ya EAC kwa kuusaini mkataba huo na kuufikisha bungeni kwa ajili ya kuridhiwa.
Lakini nchi moja kati ya sita za EAC isipouridhia, mkataba huo hautatekelezeka. Wataalamu hao waliilaumu Kenya kuwa mchawi kwa Tanzania kuingia kwenye mageuzi ya viwanda tangu mwaka 1964, 1976 na sasa mwaka 2016.
Wataalamu hao waliouchambua mkataba huo ni pamoja na Mhadhiri wa UDSM, Profesa Palamagamba Kabudi, Dk John Jingu na Dk Ng’wanza Kamata, ambao kwa nyakati tofauti walisema mkataba huo una maneno mazuri yasiyokuwa na nyenzo wala masharti chanya ya kuyatekeleza.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP