KATIKA kuendelea kujenga dhana ya kubana matumizi ya fedha za serikali, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesafiri kwa ndege ya abiria ya Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) kutoka Dar es Salaam kwenda Mwanza na kuokoa zaidi ya Sh milioni 33.

Kabla ya kuanza safari hiyo jana kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, Makamu wa Rais akizungumza na waandishi wa habari, alisema kwa kupanda ndege hiyo ameokoa fedha za serikali na kodi za wananchi.
Alisema ameona ashirikiane na Watanzania kuonesha uzalendo kwa kutumia huduma ambazo zinatolewa na serikali na kuwataka Watanzania wote kutumia ndege hizo.
“Ningepanda ndege ya kukodi ningetumia shilingi milioni 40 kwa safari hii, lakini nikaona hapana nikaamua mimi pamoja na msafara wangu tutumie ndege hii ya Shirika la Ndege Tanzania ambapo tumetumia Shilingi milioni 7.6 pekee,” alisema Makamu wa Rais aliyeambatana na watu 16 katika safari hiyo.
Makamu wa Rais ambaye alipanda ndege hiyo pamoja na abiria wengine wa kawaida, aliwataka viongozi wengine pia kufuata mfano huo kusafiri kwa kutumia ndege za shirika hilo.
Alisema ameona kwenye televisheni watu wakitoa maoni yao juu ya kampuni hiyo ya ndege kuwa ni nzuri kwa sasa na yeye akaamua kusafiri na ndege hiyo.
“Niliona kwenye televisheni watu wakitoa maoni mazuri tu juu ya shirika hili na mimi nikaona nitumie nafasi hiyo,” alifafanua Makamu wa Rais.
Hivi karibuni, serikali imenunua ndege mbili aina ya Bombardier Q400 na kuzikabidhiwa kwa ATCL na zimeanza kufanya kazi katika mikoa mbalimbali nchini huku zikiwa na gharama nafuu, lakini pia zikiwa na gharama nafuu ya uendeshaji.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ambaye alikuwepo uwanjani akimsindikiza Makamu wa Rais, alisema Watanzania waelewe kwa sasa kampuni hiyo iko kwa ajili ya kufanya biashara.
Alimpongeza Makamu wa Rais kwa kuonesha ushirikiano mkubwa na pia uzalendo kwa kusafiri na ndege ya ATCL, kwani angeweza kutumia ndege nyingine yoyote.
“Leo hii kwa kutumia ndege ya Tanzania yeye pamoja na wasaidizi wake ni jambo jema sana alilolifanya na pia ni jambo la kizalendo tunampongeza sana, kwani angeweza kutumia ndege nyingine yoyote anayoitaka,” alisema Profesa Mbarawa.
Alisema ndege za ATCL gharama zake ni nafuu na pia huduma zao zimeboreshwa zaidi, na kwamba ifikapo mwaka 2018 serikali itanunua ndege nyingine moja na pia mwaka 2019 inatarajia kununua ndege nyingine.
Profesa Mbarawa alitembelea pia karakana iliyopo katika uwanja huo wa ndege na baadaye alitembelea chuo cha mafunzo kwa wafanyakazi wa ndani ya ndege ambako alizungumza na wanafunzi waliokuwepo.
Aliwataka kufanya kazi kwa bidii kwani serikali inajenga ATCL mpya ambayo inatoa huduma bora kwa wateja wake.
“Mmekuja hapa mnaijua ATCL? Hapa tunataka watu wanaotoa huduma nzuri, ile culture (utamaduni) iliyokuwepo nyuma kama mmekuja nayo mjue mlango uko wazi hautachukua miezi sita mtaondoka. Mkifanya kazi hapa mfanye kwa bidii, mkahudumie watu kwa ukarimu kwa sababu tunataka kujenga ATCL mpya ambayo inaongoza ndege zote na hatutamvumilia mtu ambaye anaturudisha nyuma,” alieleza Profesa Mbarawa.
Aliwataka wafanyakazi hao wa ACTL kuachana na mfumo uliopita badala yake kufanya kazi kwa bidii kuijenga ATCL mpya.
Mkurugenzi Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi alisema kampuni hiyo inaboresha huduma zake ambako kwa sasa wanaboresha huduma za mtandaoni kwa ajili ya watu kushika nafasi ya safari na hata kulipia kupitia mitandao ya simu.