SPIKA Job Ndugai, amemuonya Mbunge wa Mbozi, Paschal Haonga (Chadema) kuacha kukituhumu Kiti cha Spika kuwa kinabagua kuchagua wabunge wa kuzungumza bungeni na kumwambia siku nyingine akirudia, hatamuacha salama.
Ndugai aliyasema hayo akijibu mwongozo wa Haonga na wabunge wengine jana bungeni mjini hapa. Haonga akiomba mwongozo wa Spika kwa kutumia kanuni ya 68 (7), alimtuhumu Spika kumnyima fursa ya kuuliza maswali ya nyongeza yeye na wabunge wengine wanaokaa viti vya nyuma, upande wa upinzani.

“Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na wenyeviti kila tunapotaka kuuliza maswali ya nyongeza sisi tuliokaa huku nyuma hamtuoni, wala hamtukumbuki sijui mmekula maharage ya wapi?” amesema Haonga akiomba mwongozo.
Kauli hiyo ilimfanya Spika asimame. Baada ya kusimama, alimweleza Mbunge huyo kuwa, kitendo alichofanya kumtuhumu ni kosa kubwa, kwani yeye ni kiongozi mwenye hadhi na hawezi kutuhumiwa kienyeji.
Ndugai alisema kutuhumu kiti cha spika ni sawa na mtumishi wa mahakama kumtuhumu Jaji Mkuu au ofisa wa serikali kumtuhumu Rais.
Ndugai alisema mbunge huyo amelidhalilisha Bunge.
“Kama jicho la Spika halijakuona, ntakuonaje? Kwanza wewe mweusi na umevaa suti nyeusi, ntakuonaje, siku nyingine ukirudia sitakuacha salama,” alisema Ndugai.
Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde alisimama na kueleza kuhusu utaratibu kwa kutumia kanuni ya 64 (1), na kuomba kiti kimwelekeze Haonga afute matamshi yake ya kihuni aliyoyatoa na hayana lugha ya kibunge.
Baada ya Lusinde, Ndugai alisema alimuacha Haonga aendelee kwa kuwa ni mgeni bungeni ila alisema anamwachia Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, akae naye kumpa utaratibu na maonyo.
Ndugai alisema Mbunge hawezi kujenga hoja kwa kukituhumu kiti, ni kinyume cha utaratibu na kuwataka wabunge watambue nafasi yao na kupima kauli zao.
“Tujenge utaratibu wa kuheshimiana, tuna watoto, Mheshimiwa Mbowe yupo, atakaa naye, ni maneno ya kudhalilisha, hayafai hata kidogo, ukiwa kiongozi lazima uwe kiongozi popote. Hiki ni kitu cha ovyo, tukiache.
“Mara ngapi nimekaa hapa? Haonga! Siku mbili tatu nilizokaa nimependelea nini? Tunavuka mipaka kirahisi na tunadhalilishana. Unamwambia spika amekula maharage gani? Nani kakwambia nimekula maharage?” aling’aka Spika bungeni jana.
Alisema suala hilo ana uhakika Mbowe atalifanyia kazi vizuri ili lisijirudie kwa kuwa wabunge wengi ni wageni.
Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT-Wazalendo) aliomba mwongozo kuhusu swali lililojibiwa asubuhi wakati wa kipindi cha maswali na majibu kuwa wananchi waliobomoa nyumba kupisha ujenzi wa barabara ya Mwandiga-Mwibara, hawatalipwa.
Zitto alisema wananchi hao walifuatwa na barabara na si wao walioifuata na kusema wao walibomoa kwa hiari, lakini waliokaidi na kubomolewa na serikali, walilipwa.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani akijibu swali la Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba kuhusu wananchi hao, alisema tathmini ilionesha wapo ndani ya hifadhi ya barabara. Baada ya mwongozo wa Zitto, Spika alimtaka waziri alisemee suala hilo na Waziri Profesa Makame Mbarawa alisema wamesikia ushauri wa Zitto na wataufanyia kazi.