Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba.
WAZIRI wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba amesema Tanzania inatia aibu kutokana na mbinu haramu za kuvua samaki kwa kutumia mabomu kunakofanywa na wavuvi katika bahari kuu na hivyo kuharibu mazalia ya samaki.

Ameyasema hayo Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Uvuvi yaliyoadhimishwa katika Soko la Kimataifa la Samaki la Feri na kuongeza kuwa, uvuvi haramu ni chanzo cha uharibifu wa mazingira na kuhatarisha uwepo wa rasilimali hiyo kwa vizazi vijavyo.
“Wavuvi wanaona kama uvuvi haramu ni suala endelevu kwao… hawajali kama wanaharibu mazingira ambayo yanapoteza mazalia ya samaki ambao yanahitajika hata kwa vizazi vijavyo,” alisema Dk Tizeba na kuongeza kuwa, wavuvi wengi hawana uwezo wa kufika bahari kuu jambo ambalo husababisha kutumia mabomu.
Alisema kitendo kinachofanywa na wavuvi wa aina hiyo kinasababisha Watanzania kuendelea kubakia masikini, huku wachache wakihusika kuharibu maisha ya walio wengi.
Alisema uvuvi haramu ni tatizo kubwa kutokana na wanaokwenda kinyume wakijali zaidi faida za harakaharaka, watu ambao serikali imepania kuwatokomeza.
Aliwataka wananchi kutowahifadhi wanaofanya uvuvi haramu na badala yake watoe taarifa za uhalifu huo kwani hasara yake ni kubwa kwa vizazi vijavyo.
Kuhusu ufugaji wa samaki, alisema zipo programu mbalimbali zinazohusu ufugaji wa samaki na kuwataka wananchi kwa ujumla kuzifuata taratibu ili wafuge samaki na kujipunguzia umasikini.
Akizungumzia kodi mbalimbali zinazotozwa kwa wauzaji wa bidhaa hiyo, alisema ipo haja ya kufuatilia ili mamlaka mbalimbali zinazotakiwa kudai tozo hizo ziwe zikilipiwa katika eneo moja kwa lengo la kuondoa bughudha kwa wavuvi na wadau wa samaki.