KATIKA kipindi cha mwaka mmoja kilichoanzia Novemba mwaka jana mpaka Oktoba mwaka huu ambacho kimeongozwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini Rais John Magufuli, jumla ya viwanda vipya 1,845 vimeanzishwa na hivyo kufanya jumla ya viwanda vyote nchini kufikia 54,422.

Hayo yalibainishwa hivi karibuni mjini Dodoma na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati akiahirisha Mkutano wa Tano wa Bunge la 11.
Waziri Mkuu Majaliwa alifafanua kuwa kwa mujibu wa ripoti iliyotokana na sensa ya viwanda iliyofanyika kuanzia mwaka 2013/14 hadi mwaka jana ilionekana kuwa mpaka Oktoba mwaka jana kulikuwa na viwanda 52,579.
“Ni matumaini ya Serikali kuwa kutokana na juhudi za uhamasishaji zinazofanyika, kasi ya uanzishwaji viwanda na hasa viwanda vidogo na vya kati na vikubwa itaongezeka sana,” alisisitiza Majaliwa katika hotuba hiyo ambayo hata hivyo hakuisoma bungeni kutokana na msiba wa Mbunge wa Dimani, Hafidh Ali Tahir, badala yake ikawekwa katika kumbukumbu rasmi za Bunge.
Alisema katika matokeo ya sensa hiyo hadi kufikia mwaka 2013, Tanzania ilikuwa na jumla ya viwanda 49,243 ambapo viwanda vidogo vinavyoajiri mtu mmoja hadi wanne vilikuwa ni asilimia 85.13 na viwanda vidogo vyenye watu watano hadi 49 vilikuwa asilimia 14.02.
Alisema matokeo hayo pia yalionesha kuwa viwanda vya kati vyenye watu 50 hadi 90 vilikuwa ni asilimia 0.35 na viwanda vikubwa vyenye watu kuanzia 100 na kuendelea ni asilimia 0.5.
Hivyo, Asilimia 99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo.
Alisema serikali kupitia wizara mbalimbali za kisekta tayari imebainisha maeneo mbalimbali nchini kwa ajili ya kuchochea uwekezaji kama vile kuendeleza eneo la mji wa Kigamboni na kutenga maeneo maalumu ya uwekezaji katika mikoa mbalimbali nchini.
“Hatua nyingine ni kuboresha miundombinu kama vile barabara na reli. Mfano mzuri ni ujenzi wa reli yenye urefu wa kilomita nne katika kiwanda kipya cha Kilua Group cha kutengeneza nondo kilichopo Mlandizi, Pwani,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.
Waziri Mkuu alifafanua kuwa serikali inaendelea kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa viwanda mbalimbali nchini na kwa viwanda vilivyopo karibu na bomba la gesi vitaunganishwa na bomba hilo ili vitumie gesi. Aidha, alisema tayari serikali imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha kasi ya uwekezaji kwenye sekta ya viwanda inaongezeka ili ichangie asilimia 15 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2020.
Alitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni kutambua sekta za kipaumbele kwa kuzingatia viwanda vinavyotumia malighafi za ndani, hususan kwenye sekta za kilimo na maliasili ili kuchochea uzalishaji vijiini na kuongeza ajira; kuandaa mpango mahsusi wa uwekezaji kwenye viwanda kupitia mifuko ya hifadhi ya jamii na kuhamasisha sekta binafsi, ya ndani na nje ya nchi, kuwekeza kwenye viwanda.
Alisema pia mkakati mwingine ni kutoa elimu na mwongozo kwa serikali ngazi ya mikoa na wilaya kuendelea kuhamasisha uwekezaji katika maeneo yao.