BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu nchini imetoa siku 30 kwa wadaiwa sugu ili walipe kiasi chote cha mikopo wanayodaiwa vinginevyo watawachukulia hatua kali watakaokaidi ikiwemo kuwafikisha mahakamani.
Aidha, imesema baada ya kukamilisha taratibu za kuwafikisha mahakamani wadaiwa wote sugu, watawajibika kulipa gharama za kesi na gharama nyingine za kuwatafuta.

Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru amesema jijini Dar es Salaam kuwa, hatua zitachukuliwa kwa wadaiwa wote sugu ambao hawajalipa mikopo yao, licha ya kukumbushwa kwa njia mbalimbali.
Alisema wadaiwa hao walikumbushwa kwa notisi ya Machi mwaka huu, hivyo bodi hiyo imepanga kutangaza tena majina ya wadaiwa hao sugu kwenye vyombo mbalimbali vya habari nchini na kutoa muda wa siku 30 ili walipe kiasi chote cha mikopo wanayodaiwa.
Aidha, alisema watawasilisha majina ya wadaiwa sugu kwenye Wakala wa Kumbukumbu za Mikopo ili yatumike na vyombo vingine vya fedha.
“Bodi ya Mikopo inawataka wadaiwa wote kulipa mikopo yao iliyoiva kabla hatua zaidi hazijachukuliwa. Pia bodi inawashukuru na kuwapongeza wote waliomaliza kulipa mikopo yao na wale wanaoendelea kulipa,” alisema Badru.
Alisema kumbukumbu za bodi zinaonesha kuwa jumla ya wanufaika wa mikopo 93,500 wamebainika na kupelekewa ankara za madeni yao na kati yao wanufaika 81,055 wanalipa mikopo yao na wanufaika wengine 12,445 licha ya kubainika na kupelekewa ankara na madeni yao, hawajaanza kulipa.
Alisema wanufaika 142,470 wenye mikopo iliyoiva yenye jumla ya Sh 239,353,750,176.27 hawajajitokeza na madeni yao ni ya muda mrefu na hivyo kuwafanya kuwa ni wadaiwa sugu.
“Kwa kitendo hicho wanufaika hao wamevunja sheria kama ilivyobainishwa kwenye kifungu cha sheria namba 19A(1) cha Sheria ya Bodi ya Mikopo,” alieleza Badru.
Hata hivyo, alisema kuanzia Julai, 2005 hadi Juni 30, mwaka huu, Bodi ya Mikopo imetoa Sh 2,544,829,218,662.50 kwa jumla ya wanafunzi 330,801 na hivyo kufanya jumla ya fedha zilizokopeshwa tangu mwaka 1994/1995- 2015/2016 kuwa ni Sh 2,595,932,904,575.56 na wanafunzi ni 379,179.
Alisema kati ya mikopo yote iliyotolewa mikopo iliyoiva ni Sh 1,425,782,250,734.31 iliyotolewa kwa wanufaika 238,430 ambao wamemaliza kipindi chao cha matazamio kwa kuwa mikopo hiyo hulipwa kwa kipindi cha kati ya miaka 10 na kuendelea. Hadi kufikia Septemba, 2016 mikopo iliyoiva ni Sh 427,708,285,046.48.