Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul- Razaq Badru
BODI ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imebaini kuwepo kwa baadhi ya wanafunzi ambao wamewasilisha vyeti feki vya vifo vya wazazi wao ili waonekane kama ni watoto yatima; hivyo wapewe kipaumbele cha kupatiwa mkopo.
Kuwepo kwa vyeti hivyo vya bandia kumegunduliwa na bodi hiyo baada ya kupeleka nakala za vyeti vyote vya vifo ofisi ya Msajili wa Vizazi na Vifo (Rita) kwa ajili ya uthibitisho ndipo ikagundulika kuwepo kwa kasoro hizo.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul- Razaq Badru, aliliambia gazeti hili kuwa wahusika wote ambao wamewasilisha vyeti hivyo feki suala lao limekabidhiwa kwa mamlaka zinazoshughulika na makosa ya jinai.
Hata hivyo, Badru hakutaka kuingia kwa undani kuhusu suala hilo kwa maelezo kuwa bado wanaendelea na ukaguzi.
“Bado tunaendelea kuchunguza na idadi yao hapa sina, tukikamilisha tutawaita kuwaambia idadi yao,” alisema Badru na kuongeza kuwa kutokana na kasoro hizo, ndio maana kuna baadhi ya watu wanaolalamika kuwa ni yatima, lakini hawakupata mkopo. “Hayo malalamiko ya kwamba kuna yatima wamekosa mikopo tumeyasikia, lakini na sisi tunajiridhisha kuwa huyu ni yatima baada ya kupata uthibitisho wa vyeti vya vifo kutoka Rita,” alisema Badru.
Aliongeza kuwa hata wale ambao ni wanafunzi wenye ulemavu, bodi hiyo haiwezi kuwaamini kama ni walemavu, bali hadi wapate uthibitisho kutoka kwa daktari wa wilaya (DMO) kuthibitisha ulemavu wa mwombaji.
Alisema baadhi ya wanafunzi ambao wanalalamika kuwa wamekosa mikopo ni wale ambao maombi yao yalikaguliwa na kukutwa na dosari kadhaa, na wakaombwa wazirekebishe kasoro hizo, lakini baadhi yao hawakufanya hivyo.
Badru alisema bodi yake baada ya kuchambua maombi ya waombaji wote; hadi sasa imeshatoa mikopo kwa wanafunzi wote wanaostahili wakiwemo yatima, walemavu, wanafunzi wanaosoma kozi za kipaumbele na wahitaji wanaosoma kozi zingine.
Akizungumzia suala la baadhi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) ambao wamekosa mikopo na kulazimika kurudi makwao, Badru alisema wanafunzi hao yawezekana ni miongoni mwa wale ambao hawakukidhi vigezo vya kuweza kupewa mkopo.
“Pale Dodoma tumetoa mkopo kwa wanafunzi wapya takribani 3,000, hivyo hao wanaoondoka kurudi nyumbani yawezekana wako kwenye kundi la wanafunzi ambao hawakukidhi vigezo vya kupewa mkopo,” alisema Badru.
Alisema sio rahisi kutoa mkopo kwa wanafunzi wote, kwani Serikal inaendeshwa kwa bajeti na mwaka huu wamechagua kusomesha wanafunzi 25,000 kulingana na bajeti iliyopo pamoja na kulingana na mahitaji ya wataalamu wanaotakiwa na kutokana na vipaumbele vyake.
Alisema anatambua kuna wanafunzi zaidi ya 10,000 ambao wamekosa mikopo na kuongeza; “lakini bajeti ya mwaka huu imeishia hapo, mwaka kesho tunaweza kuishauri Serikali iongeze fedha baada ya kuwa tumefanya tathmini uhitaji wa mikopo hiyo.”
Hata hivyo, Badru alisema kuna wanafunzi ambao wanasoma kozi za kipaumbele, lakini wazazi wao wana uwezo, hao nao hawakupatiwa mikopo licha ya kuwa kwenye kundi la wanaostahili mkopo.
“Kuna mtu anasomea udaktari, lakini wazazi wake wana uwezo, na kuna mwanafunzi anasomea sayansi ya jamii na wazazi wake ni watu wasio na uwezo, hapo lazima tuangalie mhitaji ni yupi kati ya hao wawili na ndiye tunampatia mkopo,” alisema Badru.
Alisema kuna wanafunzi wanasoma kozi za kipaumbele baadhi yao hawakupata mkopo kabisa na baadhi yao wamepatiwa mkopo kidogo baada ya bodi hiyo kufanya tathmini ya hali ya uchumi ya wazazi au walezi wa mwombaji.
Dodoso la wanafunzi
Akizungumzia tamko lililotolewa na Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu (TAHLISO) ambalo linahamasisha wanafunzi wasijaze dodoso lililotangazwa kutolewa na bodi yake, Badru alisema hakuna haja ya wanafunzi hao kulihofia kwa kuwa halijawekwa kwenye tovuti na bodi hiyo.
Alisema bado wanashauriana na wadau wakiwemo viongozi wa wanafunzi hao na likiwa tayari wataliweka. Alisema lengo la dodoso hilo ni zuri, kwani lina lengo la kuweka taarifa sahihi zinazohusu wanafunzi hao.
“Mwanafunzi anaweza kuwa amefiwa na wazazi wake wakati yuko mwaka wa pili, bodi itajuaje kama kuna mwanafunzi kwa sasa ni yatima? Hapo ndipo kuna ulazima wa kupitia upya taarifa za mnufaika wa mkopo,” alisema Badru.
Tahliso ilitoa tamko la kuwataka wanafunzi kugomea kujaza dodoso hilo, baada ya Heslb kutangaza kuwa inataka kupitia upya taarifa za wanufaika wa mkopo na kutathmini hali ya uchumi ya waombaji hao ili wale ambao walipatiwa mkopo kwa makosa wapokwe mkopo huo.
Baada ya tangazo hilo, Tahliso ilisema uamuzi huo wa bodi unakiuka mkataba ambao waombaji hao waliwekeana na bodi hiyo wakati wanakwenda kuomba mkopo. Shirikisho hilo pia lilidai kuwa kwa kuwa lengo la dodoso hilo ni kuwapoka mikopo baadhi ya wanafunzi, hakuna haja ya kulijaza kwani halina manufaa kwao.
Hata hivyo, Badru akizungumza na gazeti hili, alisema dodoso hilo lazima wanafunzi hao walijaze kwani lina nia njema, “Kwa nini tunapambana kabla ya jambo lenyewe kuwekwa, wasubiri wataliona.”
Jumla ya wanafunzi 65,000 wamedahiliwa kujiunga na vyuo vya elimu ya juu nchini mwaka huu.Hata hivyo, Badru anasema idadi kubwa ya wanafunzi hawakuwa na sifa wakiwemo
wale ambao hawakuomba mkopo, wenye miaka 30, waliosoma Stashahada na wengine wanasomeshwa na sekta binafsi.