Ofisa Mwandamizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Veneranda Malima(Picha ya mtandao)
IKIWA ni zaidi ya siku 10 zimepita tangu Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), kutangaza hadharani majina 142,000 ya wadaiwa sugu wa mikopo ya elimu ya juu wanaodaiwa Sh bilioni 239, wadeni hao wamejitokeza na kuanza kulipa.
Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam, Ofisa Mwandamizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Veneranda Malima, alisema tangu watoe tangazo la wadaiwa hao, kila siku hupokea wadaiwa 300 wanaokwenda kuchukua taarifa za madeni yao na wameanza kulipa.

“Ni kweli kabla ya kutoa majina ya wadaiwa hao, Novemba 4, mwaka huu pia tulitangaza kuwa tutachapisha majina ya wadaiwa hao ifikapo Novemba 14, mwaka huu na baada ya tangazo kutoka tulianza kupokea wadaiwa wengi waliokuja kuangalia taarifa za madeni yao na wameshaanza kulipa”, alisema Malima.
Akizungumzia kiasi cha malipo kilicholipwa ndani ya muda huu tangu kutangazwa kwa tangazo hilo, Malima alisema taarifa rasmi ya kiasi cha fedha kilichokusanywa kwa takribani siku 10 hadi 13, tangu watoe tangazo hilo, kitatolewa baada ya wahasibu kupitia hesabu kuona kiasi cha fedha kilicholipwa benki.
“Kuhusu idadi ya fedha tutatoa taarifa baadaye kidogo, kwa sababu hivi sasa wadaiwa wanaendelea kulipa madeni yao kupitia akaunti ya bodi ya benki, na wahasibu wetu watapitia kuona hadi sasa kwa kipindi cha wiki moja ni kiasi gani kimelipwa”, alisema Malima.
Akizungumzia madeni ya wadaiwa hao, Malima alisema yapo tofauti kulingana na aina ya kozi, muda na kiwango cha mkopo alichopewa na kuwataka wale ambao bado hawajaitikia mwito huo, kuhakikisha wanafuatilia madeni yao na kuyalipa.
“Tulichopanga ni baada ya ule muda wa siku 30 kumalizika, ambao unaisha Desemba 13, hatua zaidi tutazichukua na hatua zenyewe zinajulikana kama sheria ya mikopo hiyo inavyoeleza,” alisisitiza Malima.
Awali bodi hiyo iliwapa siku 30, kuanzia Novemba 14, mwaka huu wadaiwa sugu 142,000 wa mikopo kutoka bodi hiyo kulipa madeni yao, vinginevyo watakamatwa ili kulipa madeni yao na pia watalazimika kulipa gharama za kuwatafuta.
Hata hivyo, Novemba 14, Bodi hiyo ilitangaza hadharani majina 142,000 ya wadaiwa sugu kuanzia mwaka 1994 hadi sasa waliohitimu vyuo mbalimbali na kutolipa mikopo yao.
Tangu serikali ianze kukopesha wanafunzi, inadai Sh trilioni 2.6 kutoka kwa wadaiwa ambao walikopeshwa kwa ajili ya masomo ya elimu ya juu, lakini hadi sasa hazijarejeshwa hivyo kuleta changamoto kwa waombaji wapya.