WATU wanne wamehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kila mmoja baada ya kutiwa hatiani kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha huku wengine wanne wakiachiliwa huru kutokana na kukosekana ushahidi.
Waliopewa adhabu hiyo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Urambo, Hamis Momba ni Juma Hilya, Moses Chiza, Mihambo Masanja na Charles Mabala waliokuwa wanakabiliwa na kesi tatu tofauti.

Kabla ya kutoa adhabu hiyo, Hakimu Momba aliwaachilia huru Esta Kija, Pili Masanja, Maligita Raban na George Moses kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa kuwatia hatiani kuhusu uhalifu huo.
Katika kesi ya kwanza iliyokuwa inawahusisha watuhumiwa watano, Hakimu Momba aliwahukumu kifungo cha miaka 30 jela Juma Hilya, Moses Chiza na Mihambo Masanja kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha.
Awali ilidaiwa na Mwendesha Mashitaka, Mkaguzi wa Polisi, Philibert Pimma kuwa Mei 23, mwaka huu saa nane usiku kijiji cha Kaswa, washtakiwa wakiwa na bunduki mbili aina ya Short gun na gobori walivamia nyumbani kwa Norbet Seleste na kumpora Sh 1,860,000.
Washitakiwa Juma Hilya na Mihambo Masanja walihukumiwa tena kwenda jela miaka 30 baada ya mahakama hiyo kuwatia hatiani kwa kosa lingine la unyang'anyi wa kutumia silaha walilotenda Mei 10, mwaka huu ambapo walipora fedha taslimu Sh 4,440,000 mali ya Nchilula Elias ambaye ni mkazi wa kijiji Meza, wilaya ya Urambo.
Mahakama hiyo pia ilimhukumu kutumikia adhabu ya kifungo cha miaka 30 jela Charles Mabala baada ya kumtia hatiani kwa kosa la unyang'anyi wa kutumia silaha kosa ambalo alitenda Julai 19, mwaka huu.
Awali, upande wa mashitaka ukiongozwa na Mkaguzi wa Polisi, Phillibeth Pimma aliiambia mahakama hiyo kuwa siku hiyo saa moja usiku katika kijiji cha Songambele alipora pikipiki namba MC 492 AUN, simu mbili za mkononi na fedha taslimu Sh milioni moja mali ya Seleman Almas na kabla ya wizi huo alimtishia kumpiga risasi kwa bunduki.