Katika kusherekea siku ya Maulid ya kuzaliwa Mtume Muhammed (S.A.W), Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali itaendelea kuwatumikia Watanzania wote bila kujali imani zao za kidini.
Majaliwa ameyasema hayo katika sherehe za kitaifa za Maulid ambazo zimefanyika mkoani Singida na kusema kuwa kuna matukio ambayo yamekuwa yakijitokeza katika jamii na katika kuyachukulia hatua za kisheria vitendo hivyo Serikali haitakuwa ikibagua mtu kutokana na imani yake ya kidini kama jinsi inavyofanya kwa shughuli za maendeleo.
“Serikali inawashukuru sana kwa kuendelea kuunga mkono jitihada ya Serikali ya Rais Magufuli, tunaamini juhudi tunazofanya za kuweka nidhamu kwa watumishi wa umma na taasisi binafsi mtaendelea kutuunga mkono, tutaendelea kuruhusu uhuru wa kuabudu na kushirikiana na viongozi wa dini lakini tu mafundisho yanayotolewa yasikiuke sheria na kanuni za nchi,

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Alhaj Abukary Zubeiry Bin Ally baada ya kuwasili Shelui mkoani Singida kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Maulid Desemba 12, 2016. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dkt. Rehema Nchimbi.
“Serikali ipo macho kupambana na tukio lolote lenye nia ya kupoteza amani ya nchi yetu, Watanzania tushirikiane kutoa taarifa ili hatua zichukuliwe, ni vyema mtambue ninyi kama viongozi na waumini ndiyo walinzi wa nchi yetu, niwambie tu kuwa Serikali itaendelea kuwatumikia Watanzania wote bila kujali dini ya mtu wala kabila,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba baada ya kuwasili Shelui mkoani Singida kuwa mgeni rasmi katika Baraza la Maulid Desemba 12, 2016. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba. Muungano na Mazingira.
Nae Mufti Mkuu wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeiry amesema “Jambo ambalo Waislamu tunatakiwa kuwa nayo ni kupendana, tufanye kama Mtume wetu, yeye alikuwa akijenga mshikamano, akijenga upendo akijenga umoja na kama tunataka kumfata tumwige Mtume katika kupendana, tuache majungu, fitna na tuache kila kitu kisicho na faida,

Baadhi ya washiriki wa Baraza la Maulid wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia Baraza hilo , Shelui mkoani Singida, Desemba 12, 2016. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
“Kwanini mnagombana Waislamu na nyie ni watu wa Mungu, Waislamu tuwe na mshikamano kama tuliokuwa nao, pia tunao undugu wa Tanzania, tupendane kama Watanzania na mwenyezi Mungu ametwambia tusibague hata kama sio Waislamu, Mungu hakatazi mtu kumtendea wema mtu mwingine kama tu hakufanyi mabaya na hayo ndiyo mafunzo ya Uislamu.”