Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Dec 21, 2016

CCM Arusha wamshangaa Lowassa

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Arusha Mjini, kimeshangazwa na kauli iliyotolewa na aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa ya kumkejeli Rais John Magufuli kwa uamuzi wa kununua ndege.
Katibu wa Siasa na Uenezi Wilaya ya Arusha, Jasper Kishumbua amehoji mbona Lowassa alikuwa Waziri wa Maji na Mifugo, lakini alishindwa kutatua tatizo sugu la maji lililopo ndani ya Mkoa na Wilaya ya Arumeru.

Kishumbua ameyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu ziara aliyoifanya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Mkoani Arusha.
Amesema uamuzi wa serikali kununua ndege ni mzuri na umezingatia maslahi katika sekta ya usafirishaji na kwamba, si sahihi kiongozi aliyewahi kushika nafasi kubwa ya uongozi nchini kumkejeli Rais Magufuli.
Kishumbua amesema CCM Wilaya inamtaka Lowassa kuacha kuhubiri siasa za ulaghai huku akijua kuwa kazi iliyofanywa na uongozi wa awamu ya tano ndani ya mwaka mmoja, imewakuna na kukonga moyo wa watanzania wengi bila kujali itikadi zao na hata nje ya mipaka ya Tanzania.
Amesema, Majaliwa ametatua kero za wafanyabiashara ya usafiri wa Noah zinazofanya safari zake Arusha hadi Namanga au Arusha hadi Karatu kwa kuagiza uongozi wa Mkoa kusimamia taratibu ili magari hayo yatoe huduma bora, na kwamba, kiongozi huyo pia amesisitiza watumishi wa umma kutoa huduma kwa wananchi bila kujali itikadi zao.

Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP