MATUMIZI ya njia za asili za uzazi wa mpango ni makubwa zaidi katika mkoa wa Dar es Salaam ikilinganishwa na mikoa mingine.
Matokeo muhimu ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria Tanzania wa mwaka 2015/2016(TDHS-MIS), yameonesha kwamba mkoa huo unaongoza kwa asilimia 18.3 katika matumizi hayo ya asili ya uzazi ikifuatiwa na Mjini Magharibi, kwa asilimia 15.5 na Iringa asilimia 14.5.

Aidha mikoa yenye matumizi madogo ya njia za asili za uzazi wa mpango chini ya asilimia mbili ni pamoja na Tabora yenye asilimia 1.4, Mtwara na Mwanza zote zikiwa na asilimia 1.8 na Geita asilimia 1.9.
Utafiti huo umefanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar kwa kushirikiana na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Tanzania Bara na Wizara ya Afya kwa Zanzibar.
Akiwasilisha matokeo hayo, Meneja wa Takwimu za Jamii kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Sylvia Meku, alisema kuwa njia za asili zinazoongoza katika mkoa huo ni njia ya kuhesabu siku (kalenda) ambayo ni asilimia 12.4 ikifuatiwa na njia ya kukatisha mshindo au kumwaga nje ambayo ni asilimia 5.9.
Hata hivyo, alisema kwa ujumla matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango ni ya juu katika maeneo ya mijini kwa asilimia 35 kuliko maeneo ya vijijini ambayo ni asilimia 31 ikiwa ni tofauti ya asilimia nne. Meku alisema matumizi ya njia za kisasa yapo juu kabisa mkoani Lindi kwa asilimia 52 na yapo chini kabisa katika mkoa wa Kusini Pemba wenye asilimia saba.
Alisema matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango kwa wanawake walioolewa yanaongezeka sambamba na kuongezeka kwa utajiri wakati asilimia 35 ya wanawake walioolewa katika kaya tajiri sana hutumia njia za kisasa kwa asilimia 20 tu.
Alisema matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango yameongezeka zaidi ya mara nne tangu utafiti wa kwanza wa TDHS, kutoka asilimia saba mwaka 1991-1992 hadi asilimia 32 mwaka 2015-2016.
“Ukuaji huu wa matumizi ya njia za uzazi wa mpango ulitokea kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita ambapo matumizi ya njia za uzazi wa mpango miongoni mwa wanawake walioolewa yalikuwa ni asilimia 20 katika utafiti wa mwaka 2004-2005 TDHS,” alisema.
Asilimia uzazi wa mpango Alisema matumizi ya sasa ya uzazi wa Mpango yanaonesha kwamba takribani wanawake wanne kati ya 10 ambao ni sawa na asilimia 38 walioolewa wenye miaka 15-49 kwa sasa wanatumia njia yoyote ya uzazi wa mpango huku asilimia 32 wakitumia njia ya kisasa na sita wanatumia njia za asili.
Meku alisema njia ya kisasa inayotumika zaidi kuliko zote ni sindano kwa asilimia 13 ikifuatiwa na vipandakizi kwa asilimia saba na vidonge kwa asilimia sita. Aidha, utafiti huo unaonesha kwamba miongoni mwa wanawake wenye miaka 15-49 wanaojamiiana na ambao hawako katika ndoa, matumizi ya uzazi wa mpango ni ya kiwango cha juu.
“Zaidi ya nusu ambayo ni asilimia 54 ya wanawake hao wanatumia njia yoyote ile ya uzazi wa mpango, asilimia 46 wanatumia njia za kisasa na asilimia nane wanatumia njia za asili,” alisema.
Alisema mipira ya kinga (kondomu) ya kiume na sindano ni njia zinazotumiwa zaidi na wanawake katika kundi hilo kwa asilimia 15 kila moja ikifuatiwa na vipandikizi ambavyo ni asilimia nane na vidonge asilimia sita.
Kuhusu Dar es Salaam kuongoza kwa mpango wa uzazi wa asili na sababu, Meku alisema utafiti mwingine hasa kwa mikoa inayoonesha kuwa na asilimia kubwa ya matumizi ya njia za asili za uzazi wa mpango unahitajika ili kubaini ni kwanini wanawake wengi wanapendelea njia hiyo kuliko njia za kisasa.
Watu wanasemaje?
Hata hivyo, gazeti hili lilifanya mahojiano na baadhi ya wanawake na wanaume waliopo kwenye ndoa na kubainisha kwamba wanatumia njia tofauti katika kuhakikisha wanajikinga kupata mimba zisizotarajiwa.
Akizungumzia hilo, Sophia Nelson alisema kuwa anatumia njia ya asili ya kalenda baada ya kubaini kuwa njia za kisasa zina madhara kwake.
“Mimi niliwahi kutumia vidonge nikawa napata shida ya mzunguko wangu wa siku unaharibika, hivyo baada ya kuacha nikaona mzunguko wangu umerejea katika hali ya kawaida,” alisema.
Kwa upande wake, Hawa Salim alisema yeye hutumia njia ya uzazi wa mpango wa kisasa na ameweka vipandikizi kwa miaka sita na hajaona madhara yoyote badala yake anaifurahia ndoa yake.
Naye David John alisema kuwa wamekuwa wakitumia njia ya uzazi wa mpango wa asili na mke wake kwa kufuata kalenda na wakati mwingine inapolazimika hufanya mshindo nje.
Gazeti hili pia lilimtafuta mtaalamu wa afya ya uzazi ambaye hakutaka jina lake litajwe wala kituo chake cha kazi na kubainisha kwamba njia za uzazi wa mpango za kisasa ni nzuri na salama kama mtu atafuata ushauri wa wataalamu, lakini huwa na madhara kwa ambao hawajafuata ushauri.
“Wapo watu wanaolalamika kwamba njia za uzazi wa mpango za kisasa zina madhara, hii si kweli... nawashauri mtu unapotaka kuzitumia ufike kwenye vituo vyetu na uonane na mtaalamu kwa ajili ya vipimo na ushauri ndipo uanze kutumia njia hizi lakini mtu anapoamka na kuanza kutumia bila uchunguzi anaweza kuona kwamba njia hizi ni mbaya,” alisema.
Dar wana kila sababu
Gazeti hili lilibaini pia kuwa kutokana na maendeleo ya teknolojia, elimu nyingi ya matumizi ya njia za asili imeeleweka kwa wakazi wa Dar es Salaam na pia uelewa wao kutokana na elimu na nidhamu katika tendo la ndoa, vinawasaidia.
Aidha, pamoja na elimu hiyo inayotolewa, pia imebainika kuwa baadhi taasisi zikiwemo za dini, imani zao haziruhusu waumini wao kutumia njia za uzazi wa mpango wa kisasa na hivyo kuwaelimisha namna bora ya kutumia njia za uzazi za asili ikiwemo kufuata kalenda.
Miongoni mwa dini Waislamu na wakristo. Kwa wakatoliki, inaaminika kuwa matumizi ya njia za uzazi wa kisasa zinazowataka watu waweke vitanzi, ameze vidonge baada ya kujamiiana na kuweka vijiti, ni sawa na kuua hivyo wamekuwa na madarasa Msimbazi Center na maeneo mengine ya majimbo yake kote nchini kuelimisha waumini wao namna bora ya kutumia njia za uzazi wa mpango wa asili.
Imani hiyo inaeleza kuwa, mbegu ya mwanaume inapokutana na yai la mwanamke tayari uzima unatungwa na kiumbe ambacho ni binadamu kinakuwa kiumbe hai tangu dakika hiyo.
Baadhi wa wanandoa watatu waliozungumza na gazeti hili wa kanisa hilo, walithibitisha kufundishwa hivyo na kutumia njia ya asili kwa muda wa zaidi ya miaka 15 kwa mafanikio makubwa.