Kaimu Mkurugenzi wa Tan-Trade, Edwin Rutageruka
MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) inajiandaa kuanzisha Sabasaba Bonanza ili watu wasio na maeneo ya kufanya biashara, wakiwemo machinga, kutumia Viwanja vya Maonesho ya Biashara vya Mwalimu J. K Nyerere maarufu Sabasaba, kufanya biashara zao.

Kaimu Mkurugenzi wa Tan- Trade, Edwin Rutageruka alisema jana kuwa TanTrade itaanzisha bonanza angalau mara moja kwa wiki lakini kabla ya kufanya hivyo, watafanya utafiti wa kuanzisha Sabasaba bonanza ili watu ambao hawana maeneo ya kufanyia biashara wakauze bidhaa zao katika eneo hilo.
Rutageruka aliwataka watu ambao wanataka kuingia katika mfumo huo wa Sabasaba bonanza wafike hapo kuandikishwa.
"Tumekuwa na changamoto ya kuutumia uwanja huu kwa mwaka mzima, lakini tunataka kuanzisha Sabasaba bonanza na tumeongea na viongozi mbalimbali namna gani tutaitumia siku ya Jumamosi watu waje wauze bidhaa zao hapa," alisema.
Rutageruka aliwataka watu ambao wanataka kuingia katika mfumo huo wa Sabasaba bonanza wafike hapo kuandikishwa. Aidha alimuomba katibu mkuu huyo kuzungumza na katibu mkuu wizara ya elimu kuweka maneno yenye kuhamasisha wanafunzi katika salamu ili kujenga utamatuni wa kununua bidhaa za ndani kwa watoto.
Aliwaasa Watanzania kuinua sekta hiyo ya viwanda waendelee kuwa na uzalendo wa kununua bidhaa zinazozalishwa hapa nchini.
Hivi karibuni baada ya machinga kuondolewa katika maeneo walikokuwa wakifanyia biashara zao jijini Mwanza, Rais John Magufuli aliagiza mamlaka zote nchini kutowahamisha wafanyabiashara hao kabla ya kuwaandalia utaratibu na kuwatengea maeneo yenye miundombinu stahili kwa biashara zao.
Katika hatua nyingine, Serikali imesema inatarajia kuanzisha benki ya maendeleo ya viwanda kwa ajili ya kutoa mikopo kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza sekta hiyo.
Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhem Meru, aliyasema hayo alipokuwa akifunga maonesho hayo ya viwanda vya ndani yaliyoandaliwa na Wizara hiyo kwa kushirikiana na TanTrade. Dk Meru alisema, "Nakumbuka wakati tunaingia kwenye harakati za kilimo ilianzishwa benki ya kilimo, sasa tunaingia kwenye viwanda tunahakikisha kwamba tuna benki inayoshughulikia maendeleo ya viwanda".
Alisema watanzania wanahitaji kupata mikopo ili waweze kuanzisha viwanda na kwamba kwa kutambua hilo Serikali inalifanyia kazi kuendeleza sekta ya viwanda.
Aliwapongeza wenye viwanda hapa nchini kwani wameboresha bidhaa zao ambazo zina viwango vya kitaifa na pia kimataifa ambapo amewataka jitihada zao kujielekeza pia katika kutanua masoko ya ndani na nje ya nchi.