Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Dec 12, 2016

Wataka kitendawili cha maiti Ruvu kiteguliwe


Mwenyekiti wa UTG, Malisa Godlisten
SERIKALI imeshauriwa kutokaa kimya kuhusu chanzo cha vifo vya watu saba ambao miili yao ilikutwa katika mifuko ya sandarusi katika kingo za Mto Ruvu, wilayani Bagamoyo, Pwani.
Aidha imeelezwa kuwa mazingira ya kutatanisha ya kupotea kwa mfanyakazi wa ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benard Saanane lazima kutazamwe.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Umoja wa Kizazi cha Kuhoji Tanzania (UTG), Malisa Godlisten jana jijini Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu matukio hayo.
Alisema serikali kwa kushirikiana na taasisi zake ikiwemo wizara hiyo ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto na Ofisi ya Mkemia Mkuu inapaswa kuratibu kazi ya kufukuliwa kwa miili ya watu hao saba iliyookotwa na kuzikwa eneo la Mto Ruvu, ili kupata sampuli zitakazotumika kutambua ndugu wa marehemu watakapojitokeza na chanzo cha vifo hivyo.
Miili ya watu sita ilikutwa Desemba 7 mwaka huu kando ya mto Ruvu wilayani humo ndani ya mifuko ya sandarusi na ndani ikiwa imewekwa mawe ili isielee kisha mifuko hiyo kushonwa kama mzigo wa mazao na kutupwa mtoni.
Mwili mwingine uliokotwa Desemba 9 mwaka huu eneo hilo hilo na pamoja na kutokuwa katika mfuko wa sarandusi, ulikuwa umevuliwa shati na kuonekana na majeraha mgongoni na kwenye ubavu umekatwa na kitu chenye ncha kali.
Mwishoni mwa wiki, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Boniventure Mushongi alisema miili yote ilizikwa kwa kuwa ilikuwa vigumu kuwatambua kutokana na kuharibika vibaya huku kukiwa hakuna kitambulisho chochote kinachoashiria watu hao ni nani na wametoka wapi na kwamba Polisi inaendelea na upelelezi kubaini waliohusika na mauaji hayo, atakayebainika sheria itachukua mkondo wake.
Aidha kuhusu kupotea kwa Saanane, Godlisten alisema UTG inaipa Chadema saa 72 kutoa taarifa ya kupotea kwa Saanane aliyeondoka nyumbani kwake Novemba 18 mwaka huu hadi leo hii hajaonekana wala taarifa zake kutolewa sehemu yoyote.
Alisema tukio la kupotea kwa Saanane aliyekuwa akifanya kazi Makao Makuu ya Chadema, Dar es Salaam, lilianza kuibua mijadala kuanzia Novemba 26 mwaka huu baada ya kutoonekana nyumbani kwake Tabata na eneo lake la kazi.
Alisema akiwa Katibu wa umoja wao huo, baada ya kutojulikana alipo wakishirikiana na familia yake walikwenda eneo alilokuwa akifanyia kazi na kuulizia, baada ya kukosa taarifa walitoa taarifa Makao Makuu ya Polisi na kituo cha Polisi Tabata, Desemba 5 mwaka huu na kupewa RB namba TBT/RB/8150/2016, ambapo pamoja na mambo mengine walipewa ruhusa ya kumtafuta maeneo mbalimbali.
Alisema walianza kumtafuta maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam ikiwemo hospitali za Amana, Temeke, Mwananyamala na Hospitali ya Taifa Muhimbili, walipewa ushirikiano wa kutosha kwa kukagua vyumba vya wagonjwa mahututi, orodha ya wagonjwa waliolazwa wasiotambulika na katika nyumba za kuhifadhi maiti bila mafanikio.
Alisema baada ya kumkosa walitoa mrejesho polisi na kuomba wawasiliane na vituo vyao ili kujua kama ameshikiliwa mahabusu wakaambiwa hajashikiliwa wakaomba kujiridhisha kwa kupita katika vituo hivyo na kuvikagua.
“Kati ya Desemba 6 na 7 mwaka huu tukapita na kukagua mahabusu katika vituo vyote vikubwa vya Polisi jijini Dar es Salaam vikiwemo Kituo cha Polisi Oysterbay, Mabatini, Urafiki, Magomeni, Buguruni, Chang’ombe na kiutuo cha polisi Sitaki Shari lakini hatukufanikiwa kumpata katika vituo hivyo, wala hakuwemo katika orodha ya mahabusu waliowahi kufikishwa katika vituo hivyo,” alisema.
Godlisten alisema baada ya hapo walienda kuuliza katika magereza mawili jijini Dar es Salaam yanayohifadhi mahabusu la Segerea na Keko bila mafanikio. Vile vile Ofisi za Uhamiaji Uwanja wa Ndege jijini Dar ili kujua kama amekwenda nje ya nchi wakagundua hajasafiri nje ya nchi.
Alisema ili kujiridhisha zaidi walikwenda Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ili wapate taarifa za mawasiliano ya mwisho ya Saanane kuwasaidia kutambua alipo huko wakaelezwa jukumu hilo ni la kampuni ya simu kupitia jeshi la polisi hivyo polisi inapaswa kuandika barua TCRA kuomba taarifa hizo.
Alisema polisi walichukua maelezo upya ya tukio hilo na kuahidi kuandika barua hiyo kwenye mtandao husika wa simu ili kupata mawasiliano hayo, lakini hadi sasa hawajapata mawasiliano hayo.
Alisema baada ya jitihada zote hizo kufanyika bila mafanikio, Desemba 8 mwaka huu ziliripotiwa taarifa za kuokotwa kwa miili ya watu huko Bagamoyo eneo la mto Ruvu, ambapo walisafiri kwenda kujiridhisha kama yupo miongoni mwa maiti hizo, lakini walikuta miili yote imeshazikwa bila kuacha kielelezo chochote.
Alisema wanasikitika kuona vifo vya watanzania vikipewa uzito mdogo na taasisi zenye wajibu wa kushughulikia jambo hilo. “Ni ajabu hadi kamati ya ulinzi na usalama mkoa wa Pwani haijachukua hatua zinazoridhisha juu ya jambo kubwa kama hili.
Taarifa tuliyoipewa kutoka ofisi ya kata inaeleza kuwa hadi kufikia tarehe 10 mwezi huu hakuna kiongozi yeyote wa serikali kuu aliyekuwa amefika eneo hilo. Si waziri, mkuu wa mkoa wa Pwani wala mbunge wa eneo husika,” alisema.
Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP