Rais John Magufuli
RAIS John Magufuli amefanya uteuzi wa mabalozi 21, wateule wakiwa 15, kujaza nafasi zilizowazi katika Balozi za Tanzania zilizopo katika nchi mbalimbali wakiwemo wanasiasa mashuhuri, Dk Emmanuel Nchimbi, Sylvester Mabumba, Omar Yusuf Mzee, Dk Pindi Chana na Rajab Luhwavi.
Aidha, ameteua mabalozi wengine sita kuiwakilisha Tanzania katika balozi mpya sita ambazo zitafunguliwa hivi karibuni katika nchi za Algeria, Israel, Korea ya Kusini, Sudan, Qatar na Uturuki.

Taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi jana ilisema mabalozi wateule ambao watapangiwa vituo vya kazi baadaye ni katika nchi za China, Ufaransa, Makao Mkuu ya Jumuiya ya Nchi za Ulaya, Oman, Italia, India, Afrika Kusini, Kenya, Brazil, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Nigeria, Comoro na Umoja wa Mataifa.
Kijazi aliwataja mabalozi waliteuliwa kuwa ni Balozi Mbelwa Kairuki, Balozi Samuel Shelukindo, Balozi Joseph Sokoine, BaloziSilima Haji, Balozi Abdallah Kilima, Balozi Baraka Luvanda na Balozi Dk James Msekela.
Pia aliwataja mabalozi wateule kuwa ni Sylvester Ambokile, Dk Chana, Dk Nchimbi, Luhwavi, Luteni Jenerali Mstaafu Paul Mella, Grace Mgovano, Mohamed Said Bakari, Job Masima, Mzee, Matilda Masuka, Fatma Rajab, Mabumba, Profesa Elizabeth Kiondo na George Madafa ambaye uteuzi wake ulishatangazwa.
Wakati Nchimbi ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na waziri mwandamizi wa zamani, Dk Chana pia ameshikilia nafasi hiyo ya ujumbe wa Kamati Kuu ya CCM kwa muda mrefu, lakini pia aliwahi kuwa naibu waziri katika serikali ya awamu ya nne, huku Luhwavi akishikilia nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara.
Wanasiasa Mabumba na Mzee ni maarufu kwa siasa za Zanzibar na Bara, ambapo Mabumba amewahi kushikilia nafasi ya Mwenyekiti wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Bunge la 10, huku Mzee akishikilia nafasi ya uwaziri katika pande zote za Muungano, mara ya mwisho akiwa Waziri wa Fedha na Uchumi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kijazi alisema mabalozi wote waliobaki katika vituo ambavyo si kati ya vituo hivyo 15 vilivyotajwa wataendelea na nafasi zao za uwakilishi wa Tanzania katika vituo walivyopo.
Wakati huo huo, Katibu Mkuu Kiongozi alisema Rais Magufuli amemhamisha Balozi Modest Mero kutoka kituo chake cha sasa cha Geneva, Uswisi kwenda Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa (New York, Marekani) ambako atakuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, akichukua nafasi ya Balozi Tuvako Manongi ambaye atastaafu ifikapo Desemba 6, mwaka huu.
Pia, Rais Magufuli amemteua Grace Martin kuwa Balozi na Mkurugenzi wa Itifaki katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki jana ambapo kabla ya uteuzi huo Martin alikuwa akikaimu nafasi hiyo.
Katika panga pangua hiyo ya Mabalozi, Rais Magufuli amemteua Balozi Peter Kallaghe kuwa Ofisa Mwandamizi Mwelekezi – Mambo ya Nje katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi na kabla ya uteuzi huo Kallaghe alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza hadi mwanzoni mwa mwaka huu.