WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Kilimo,
Mifugo na Uvuvi, Charles Tizeba kufanya uchunguzi kwa nini mbolea ya minjingu
inayozalishwa nchini haitumiki na badala yake inaagizwa mbolea kutoka nje ya
nchi.

Ametoa agizo hilo jana (Jumamosi, Desemba 3, 2016) wakati
alipotembelea kiwanda cha Fibre Board 2000 Limited ambacho kinatengeneza bidhaa
mbalimbali ikiwemo mbolea ya Minjingu, wakati akiwa katika siku ya pili ya
ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.Alisema mbolea hiyo licha ya kuwa na viwango vya ubora
vinavyohitajika, haitumiki nchini kwa sababu ya kuingiliwa na masuala ya
kisiasa dhidi ya matumizi yake.

“Nchi jirani ya Kenya inaiona mbolea hii bora kuliko sisi wa
ndani? Mheshimiwa Waziri wa Kilimo are we serious? Tunazalisha
mbolea hapa tunasema haina kiwango lakini Kenya wanaitaka na wameagiza tani
300,000,” alisema.

Waziri Mkuu aliongeza kuwa “Jambo hili lazima liangaliwe
ndani ya Wizara kwa nini mnaagiza mbolea kutoka nje wakati ndani tunazalisha
hii ni mianya ya rushwa, rushwa ulaji ulaji tu. Waziri lichukulie maanani jambo
hili hatutaki siasa katika sekta ya kilimo,”.Alisema kumekuwa na mijadala mingi kuhusu mbolea ya minjingu
kumbe baadhi ya watendaji wanatengeneza mianya ya kwenda kununua mbolea nje
ambako hutumia fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika katika miradi mingine ya
maendeleo.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda cha Fibre Board 2000
Limited, Tosk Hansi  amesema kampuni hiyo inayozalisha bidhaa mbalimbali
ikiwemo mbolea ya minjingu, imetoa ajira kwa watu zaidi ya 1,800 wengi wao
wakiwa ni vijana ila inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya urasimu wakati
wanapoomba vibali vya uvunaji mazao ya misitu.


Awali, kampuni hiyo ya Fibre Board 2000 limited imemkabidhi
Waziri Mkuu mchango wa madawati 1,000 kwa ajili ya shule mbalimbali za mkoani
Arusha ili kuwawezesha wanafunzi kusoma katika mazingira mazuri.


IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU